1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund yamtaka Auba kufanya uamuzi

Bruce Amani
17 Julai 2017

Ni wazi sasa kuwa kipindi cha usajili wa wachezaji nchini China kimekamilika. Hivyo Pierre-Emerick Aubameyang atabaki Ulaya. Lakini je, atabaki Dortmund?

https://p.dw.com/p/2gg1s
Bundesliga 34. Spieltag  - Borussia Dortmund vs Werder Bremen 2:1
Picha: picture alliance/dpa/B. Thissen

Mkurugenzi wa spoti wa AC Milan Marco Fassone amesema wana fedha za kutodha kumnunua mshambuliaji mwingine kama vile Andrea Belotti wa Torino, Alvaro Morata wa Real Madrid, au Aubameyang

Lakini afisa mkuu mtendaji wa BVB Hans-Joachim Watzke amesema wamemwambia Auba kuwa kama anataka kuondoka, na ana klabu inayoweza kutimiza masharti ya BVB basi anaweza kuwaarifu. Kwa sababu BVB inahitaji kutafuta mchezaji atakayejaza nafasi yake kitu ambacho sio rahisi. Inasemekana wamempa hadi Julai 26 kufanya uamuzi.

Wakati huo huo, ripoti zinaeleza kuwa mabingwa wa Ligi ya Premier Chelsea wanaandaa ombi la euro milioni 75 kumpata mshambuliaji huyo.

Telekom Cup 2017  Renato Sanches FC Bayern Muenchen Fortuna Duesseldorf - FC Bayern Muenchen
AC Milan wanamtaka Sanches kwa mkopoPicha: picture-alliance/Sven Simon

Baada ya kukamilika sakata linalozunguka uhamisho wa Anthony Modeste nchini China, mtazamo sasa umegeukia klabu ya FC Köln kuhusu namna itatumia euro milioni 30 ilizopata kwa uuzaji wa  mshambuliaji huyo Mfaransa. Lakini mkurugenzi wa spoti Jörg Schmadkte amesema kuwa klabu hiyo haina haraka ya kuzitumia fedha hizo.

Ripoti zimeihusisha Cologne na mshambuliaji wa Hoffenheim Mark Uth lakini kocha wa Hoffenheim Julian Nagelsmann ambaye alipigiwa kura kuwa kocha bora wa mwaka amepuuza madai hayo akisema Cologne watalazimika kumtafuta mshambuliaji mwingine.

AC Milan yazungumza na Bayern kuhusu Sanches

Afisa mkuu mtendaji wa Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge amethibitisha kuwa AC Milan imewasilisha ombi la kumchukua kwa mkopo kiungo Mreno Renato Sanches mwenye umri wa miaka 19, lakini akasema kuwa mazungumzo hayo hayaendi vyema.

Sanches alijiunga na mabingwa hao wa Ujerumani msimu uliopita katika uhamisho wa euro milioni 35 kutoka Benfica lakini ameshindwa kujiimarisha katika klabu ya Munich.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Yusuf Saumu