1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC na WHO zatangaza kutokomeza Ebola mikoa mitatu Congo

John Kanyunyu25 Juni 2020

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na Shirika la Afya Ulimwenguni,wametangaza leo kutokomezwa kwa homa ya Ebola katika mikoa mitatu ya mashariki mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3eL04
Kongo: Erneuter Ausbruch von Ebola
Picha: Reuters/G. Tomasevic

Kutokomezwa huko kwa Ebola kunatokea mnamo wakati nchi hiyo inakabiliana pia na homa ya Covid-19. 

Waziri wa afya wa serikali ya Congo amewatangazia wakaazi wa mikoa ya Kivu ya Kaskazini, Kivu ya Kusini na Ituri, kutokomezwa kwa homa ya ebola, iliyowauwa watu 2277 katika eneo hili.

"Wakati huu ambao tunatangaza kutokomezwa kwa homa ya Ebola ambayo ilikuwa mlipuko wa mara ya kumi katika nchi hii, nchi yetu inakabiliana pia na mripuko mwingine wa homa hiyo Mbandaka katika mkoa wa Équateur mei thelathini na moja mwaka huu. Tunatumia fursa hii kuwahakikishia wakaazi wa mikoa ya Kivu ya Kaskazini, Kivu ya kusini na Ituri, kwamba tutabakiza kikosi kimoja ambacho kitakuwa na jukumu la kuwaelimisha watatibu wa mahali hapo,ambao kwa upande wao wataendeleza mafanikio ya vita dhidi ya ebola." Amesema waziri wa afya Eteni Lobgondo.

Tangazo la kutokomezwa kwa ebola halikutarajiwa

Kutangazwa kutokomezwa kwa homa ya ebola katika eneo hilo, hakukutarajiwa na wengi kwani, siku zilizopita,siku chache kabla ya kutangazwa mwisho wa Ebola, palijitokeza visa vya maambukizi mapya, jambo lililosababisha tume ya watabibu wanaokabiliana na ebola kuwashughulikia wagonjwa, na imani ya kutokomezwa kwa ebola kutoweka.

Picha ya maktaba: Maafisa wa afya wakimhudumia mgonjwa wa ebola katika kituo cha Katwa Butembo Oktoba 3, 2019.
Picha ya maktaba: Maafisa wa afya wakimhudumia mgonjwa wa ebola katika kituo cha Katwa Butembo Oktoba 3, 2019.Picha: Reuters/Z. Bensemra

Wakizungumza na DW, wakaazi hawa wa Beni, pamoja na kwamba wanajikinga dhidi ya homa ya Corona, wanafurahia kumalizika kwa ebola, pale wakiwa na mashaka, kwamba huenda pakajitokeza maambukizi mapya, kama ilivyokuwa awali.

Hatua za tahadhari, zimesaidia kufanikisha vita dhidi ya ebola

Wakaazi wa maeneo ya Beni na Butembo, pamoja na eneo la Mambasa katika mkoa wa Ituri, wanao uzoefu, katika kujikinga dhidi ya ebola, pale wakiwa wanaheshimu kanuni za usafi, jambo ambalo wengi wao wanalitaja, kuwa linawasaidia ipasavyo,katika kujikinga dhidi ya janga la Covid-19.

Tangu kuzuka kwa homa ya Ebola katika eneo hili mnamo mwaka wa 2018, ni watu elfu mbili mia mbili na sabini na sabaa ndio walifariki kwa Ebola,na watu elfu moja mi amoja na sabini na moja ndio walipona homa hiyo hatari, baada ya kuambukizwa.