1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Droo ya hatua ya makundi Champions League

29 Agosti 2014

Mabingwa watetezi Real Madrid watakutana na Liverpool wakati pia timu tatu za Uingereza zikishuka dimbani na wapinzani kutoka Ujerumani. Droo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imefanyika Monte Carlo

https://p.dw.com/p/1D3ps
Champions League 2014/2014 Auslosung Symbolbild
Picha: picture-alliance/dpa

Droo hiyo iliyoongozwa na wachezaji wa zamani nguli wa Real Madrid kama heshima ya ushindi wao wa taji la kumi la Ulaya maarufu kama La Decima, imewaweka katika kundi B pamoja na Liverpool, Basel wa Uswisi na Ludogorets Razgrad wa Bulgaria.

Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich watalenga kutinga fainali msimu huu, ambayo pia itaandaliwa mjini Berlin, mnamo Juni 6, 2015 katika uwanja wa Olympia, lakini ni lazima kwanza waponyoke kutoka kundi gumu la E, ambalo kama tu mwaka jana, lina mabingwa wa England Manchester City na CSKA Moscow pamoja na makamu bingwa wa Italia, AS Roma.

Kibarua cha Borussia Dortmund katika Kundi D kinajumuisha marudio ya mapambano ya msimu uliopita dhidi ya Arsenal pamoja na Galatasaray na Anderlecht. Mahasimu wa Dortmund, Schalke, pia watasafiri mjini London kukutana na Chelsea lakini pia watakuwa na Sporting Lisbon na Maribor kutoka Slovenia katika kundi G.

Champions League Auslosung 2014/2015 Monte Carlo 29.08.2014
Droo ya mechi za makundi za Ligi ya Mabingwa Ulaya ilifanyika Monte Carlo, MonacoPicha: Reuters

Atletico Madrid, ambao ni makamu bingwa wa Champions League msimu uliopita, wamepangwa katika Kundi A pamoja na Juventus, Olympiacos na Malmo, wakati Barcelona wakitumbukizwa katika Kundi F kupambana na Paris Saint Germain, Ajax na Apoel Nicosia kutoka Cyprus. Kundi C lina Benfica, Zenit St Petersburg, Bayer Leverkusen na AS Monaco wakati Kundi H likizileta pamoja timu za Porto, Shakhtar Donetsk, Athletic Bilbao na BATE Borisov kutoka Belarus.

Mechi za raundi ya kwanza zimepangwa Septemba 16/17 na hatua ya makundi itakamilika Desemba 9/10. Timu mbili za kwanza kutoka kila kundi zitafuzu katika awamu ya mchujo wakati nambari tatu wakiteremka katika Europa League:

Lakini suala ambalo huenda limezusha gumzo sana ni kuhusu namna ambavyo droo hiyo hufanyika. Mfumo wa UEFA ambao unazingatia points ambazo kila timu hujikusanyia unadhihirisha wazi ni ligi zipi zilizo imara zaidi katika dimba hilo na kwa sasa orodha hiyo ni Uhispania, England, Ujerumani, Ureno, Italia, Urusi na Ufaransa.

Hivyo katika hatua ya kuondoa hali hii ya sasa, mbona kusiwe na mfumo ambao mabingwa wa ligi hizo wanaorodheshwa na kupangwa kama timu saba kubwa pamoja na anayeshikilia kombe la Mabingwa? Na kama hivyo kwa mfano Kile chungu A kingekuwa na Atletico Madrid, Manchester City, Bayern Munich, Benfica, Juventus, CSKA Moscow, Paris Saint Germain na Real Madrid.

Kisha B kingekuwa na mabingwa wa ligi nyingine nane ndogo, kama watakuwa wamefuzu….pamoja na timu zitakazomaliza katika nafasi za pili kutoka UHISPANIA, Uingereza na Ujerumani…na kadhalika…hii inaweza kuhakikisha kuwa kuna mchanganyiko mpya kila msimu…

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu