1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dubai-na shirika la ujasusi la Israel:Mossad

19 Februari 2010

Je,mkuu wa Mossad akamatwe ?

https://p.dw.com/p/M5ZV
Avigdor LiebermanPicha: AP

Nchi 4 zaUlaya,Uingereza,Ireland,Ufaransa na Ujerumani, ambazo paspoti zao zimetumiwa na wale waliosafiri kwenda Dubai na kumua kamanda wa chama cha Wapalestina cha HAMAS, Mahmud al Mabhuh, zikiichagiza Israel kujieleza,Israel, imelikataa dai la kutaka mkuu wake wa ujasusi wa Idara ya Mossad atiwe nguvuni.

Uingereza,Ireland,Ufaransa na Ujerumani, jana ziliwaita wajumbe wa kibalozi wa Israel kwa mazungumzo katika wizara zao za mambo ya nje kujieleza juu ya kisa cha mauaji mwezi uliopita na matumizi ya pasi-bandia za nchi zao.Mauaji ya Kamanda wa chama cha Hamas Mahmud al-Mabhuh, yanadhaniwa mno ni kazi ya Idara ya ujasusi ya Israel "MOSSAD",

Wakati huo huo,Shirika la INTERPOL, limetoa hati za kukamatwa kwa watuhumiwa 11-sita kati yao wameorodheshwa kutumia pasi za Uingereza,watatu za Ireland,mmoja ya Ufaransa na mwengine ya Ujerumani.Wote hao, wanatakiwa na serikali ya Dubai,huko Falme za Kiarabu kwa mauaji hayo ya Kamanda wa chama cha Hamas.

"Tunataka kujua kiini cha mkasa huu wa kutumika kwa pasi za udanganyifu au matumizi yake hasa"-waziri wa nje wa Uingereza David Miliband alisema baada ya balozi wa Israel,mjini London Ron Prosor kufanya mazungumzo na Peter Ricketts, mkuu wa Idara ya Uingereza ya shughuli za kibalozi.

Nae waziri mkuu wa Uingereza ,Bw.Gordorn Brown, alisisitiza hapo jana haja ya kufanyika uchunguzi kamili:

"Nadhani hili ni swali la kuchunguzwa.tunapaswa kujua kilichotokea juu ya passpoti za Uingereza na ni uchunguzi unaobidi kufanywa kabla kutoa uamuzi wa mwisho."

Nae Balozi wa Israel ,mjini London alisema:

"Sikuweza kutoa taarifa zaidi juu ya ombi la Uingereza."

Taarifa kutoka Jeruselem, leo zinasema Israel, imekataa kabisa kuitikia ombi la kumkamata mkuu wake wa Idara ya Ujasusi (Mossad) kwa kuhusika na kuuwawa kwa kamanda wa chama cha Hamas.

"Polisi ya Dubai haikutoa ushahidi wazi wa kumtia hatiani." Afisa wa hadhi ya juu wa Israel aliliambia shirika la habari la Ufaransa (AFP).

Mkuu wa Polisi wa Dubai,Khalfan, alidai jana kutiwa nguvuni kwa Mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Israel (Mossad) Meier Dagan, ikibainika kuwa shirika lake ndilo nyuma kama inavyodhaniwa na wengi ya mauaji ya Bw.Mahmud al-Mabhuh huko Dubai.

Mjini Berlin, serikali ya Ujerumani nayo imedai maelezo kutoka Israel kuhusu mauaji hayo.Hii ilikuwa wakati wa mkutano kati ya afisa wa hadhi ya juu wa wizara ya nje ya Ujerumani na mjumbe wa kibalozi wa Israel.

Nae waziri wa nje wa Ujerumani Guido Westerwelle akasema,

"Kutokana na habari zilizofichuka hadi sasa,nadhani ni lazima kufafanua wazi hali zilizopelekea kuuliwa kwa bw.mahmud al Mabhuh."

Waziri wa nje wa Israel Avigdor Lieberman, anakabiliwa kwahivyo na maswali magumu Jumatatu ijayo atakapokutana mjini Brussels na mawaziri wenzake wa nje wa Umoja wa Ulaya .Ziara yake hii ilipangwa kabla ya mkasa wa mauaji wa Dubai.

Mwandishi: Ramadhan Ali /AFPE

Uhariri: Othman Miraji