1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Dunia ilishindwa kuzuia mauaji Rwanda, Bosnia"

24 Mei 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekamilisha ziara yake nchini Rwanda akisema jamii ya kimataifa haiwezi kukubali kushindwa kama ilivyoshindwa wakati wa mauaji ya Rwanda ya 1994 na ya Srebrenica mwaka 1995.

https://p.dw.com/p/18dLA
World Bank President Jim Yong Kim (L) and UN secretary general Ban Ki-moon (C) give a press conference on May 22, 2013 in Kinshasa. Ban Ki-moon wraps up a visit to Mozambique and arrives in Kinshasa on a key leg of his Africa trip centred on restoring peace in eastern Democratic Republic of Congo where a flareup in fighting over the past days has left 19 dead. AFP PHOTO/JUNIOR D.KANNAH (Photo credit should read Junior D. Kannah/AFP/Getty Images)
Ban Ki Moon und Jim Yong Kim in Kongo 22.05.2013Picha: Junior D. Kannah/AFP/Getty Images

Ban Ki-moon amesema eneo la Maziwa Makuu limekumbwa na machafuko ambayo yamegharimu maisha ya watu wengi wasio na hatia wakati jamii ya kimataifa ikiendelea kuweka mikakati isiyozaa matunda kwa miongo kadhaa sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza ziara yake nchini Rwanda akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ikiwa hali ya mambo itaendelea kuwa ilivyo sasa, basi hakuna maendeleo bila amani na wala hakutakuwa na amani bila maendeleo.

"Mchakato wa amani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na utekelezwaji wake ni ndiyo nafasi muhimu ya maendeleo endelevu ya kanda hii nzima daima. Ninawahimiza marais wote na kila mmoja kuwa kutekeleza mchakato huo na kuheshimu majukumu yao juu ya hilo."

Dunia ilishindwa Rwanda, Bosnia

Alihoji Ban Ki-moon, ambaye alikuwa wazi kwa kusema kwamba Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa walishindwa wakati yakitokea mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994 na mwaka uliofuata wakashindwa tena kwenye mauaji ya Srebrenica kwenye vita vya Bosnia-Herzegovina ambapo watu 8,000 waliuawa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, akiwatembelea wanajeshi wa Umoja huo nchini Kongo wakati wa ziara yake ya Goma,
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, akiwatembelea wanajeshi wa Umoja huo nchini Kongo wakati wa ziara yake ya Goma,Picha: Reuters

Kutokana na uzoefu huo akasema jamii ya kimataifa haiwezi kukaa kando wakati mambo yakiendelea kuharibika mashariki mwa DRC. Ban Ki Moon amesema kwamba ili kutekeleza maazimio ya kuleta amani mashariki mwa DRC ndiyo maana Umoja wa Mataifa ukatuma kikosi zaidi cha kulinda amani mashariki mwa nchi hiyo.Amekiri wazi kwamba mikataba kadhaa ya awali kuhusu DRC haikutekelezwa lakini kwamba kwa sasa wamepania.

"Mikataba kadhaa hapo awali ilisainiwa lakini haikuheshimiwa lakini wakati huu tutahakikisha tunatekeleza mikakati hii ili watu wa eneo hili waweze kuishi kwa amani na usalama bila woga."

Jana Katibu Mkuu huyo alifanya mazungumzo yaa faragha na Rais Paul Kagame na baadaye wakakutana na mawaziri mbalimbalikwenye mjadala wa pamoja.

Kwa upande mwingine Rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim, ambaye anafuatana na Ban Ki-moon, amesema Benki yake inaunga mkono michakato na juhudi kuleta amani ya kudumu kwenye eneo hilo kwa kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile miundombinu ya barabara, umeme, afya na elimu.

Tayari Benki ya Dunia imekwishatangaza kutoa dola bilioni 1 za Kimarekani kusaidia miradi hiyo.

Mwandishi: Sylvanus Karemera/DW Kigali
Mhariri: Mohammed Khelef