1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaadhimisha Vita Vikuu vya Pili katikati ya COVID-19

Mohammed Khelef
9 Mei 2020

Sherehe za kuadhimisha miaka 75 tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia zimefanyika kimya kimya kutokana na ulimwengu kukabiliwa na mzozo mbaya kabisa wa janga la virusi vya korona.

https://p.dw.com/p/3bymL
Russland Sevastopol Nationalfeiertag Ende WW2 Coronakrise Masken
Picha: picture-alliance/dpa/Sputnik/V. Batanov

Nchini Urusi, ambako kawaida sherehe hizo hufanyika kwa gwaride kubwa kabisa la kijeshi siku moja baada ya kuadhimishwa kwake kwengineko barani Ulaya, Rais Vladimir Putin amelazimika kulifuta gwaride hilo la Jeshi Jekundu na badala yake akatowa hotuba akiwa nje ya jengo la ikulu ya Kremlin mjini Moscow.

Lakini kwenye hotuba yake, Putin hakusema chochote kuhusiana na virusi vya korona, ingawa Urusi sasa inashikilia nafasi ya tano miongoni mwa mataifa yaliyoathiriwa sana na maambukizo hayo, ikiwa inarikodi wagonjwa wapya 10,000 kila siku kwa wiki nzima sasa.

Maafisa wanasema idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa imepanda kwa wengine 10,817 na hivyo kuifanya idadi jumla kuwa 198,676, hali inayoiweka Urusi nyuma ya Marekani, Uhispania, Italia na Uingereza.

Serikali inasema ongezeko hilo, miongoni mwa sababu nyengine, linatokana na kampeni yake ya kuwapima watu wengi kadiri iwezekanavyo, lakini idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na maradhi hayo ni ya chini sana inapolinganishwa na mataifa mengine yanayorikodi kasi kama hii ya maambukizo. Kufika sasa, Urusi imepoteza watu 1,827 kutokana na COVID-19.

Katika taifa jirani la Belarus, hata hivyo, maelfu ya wanajeshi walionesha ukakamavu wao kwenye gwaride lililofanyika mbele ya uwanja mjini Minsk kuadhimisha miaka 75 ya kushindwa kwa jeshi la Wanazi wa Ujerumani.

Rais Alexander Lukashenko, ambaye amekuwa akiliangalia janga la korona kwa njia tafauti, alikuwapo kushuhudia vikosi vya wanajeshi wa miguu na anga wakitowa heshima kwa taifa lao.

Malkia Elizabeth II ataka Waingereza wasikate tamaa

UK Rede der Queen zu 75 Jahre Kriegsende
Malkia Elizabeth II wa Uingereza akihutubia taifa kwenye maadhimisho ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia.Picha: picture-alliance/abacaD. Nievere

Nchini Uingereza, Malkia Elizabeth wa II alitowa hotuba jana Ijumaa (Mei 8) akiwataka wananchi kutokuvunjika moyo, ukiwa ujumbe wake wa siku itambuliwayo kama Siku ya Mashujaa.

Uingereza, nayo kama yalivyo mataifa mengine, iliadhimisha mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia bila ya shamrashamra za mitaani na magwaride ya kijeshi, ambayo yote yamefutwa kutokana na mripuko ya virusi vya korona.

"Na ninapoiangalia nchi yetu leo na kuona kile tulicho tayari kukitenda kwa ajili ya kuilinda na kusaidiana baina yetu, ninaona fahari kwamba bado sisi ni taifa la wanajeshi, mabaharia na manahodha shujaa ambao kila mtu angeliwatambua na kuwahusudu," alisema Malkia huyo mwenye umri wa miaka 94. 

Kufikia mchana wa leo (Jumamosi, Mei 9), watu walioambukizwa maradhi hayo ni 3,946,130 duniani kote, huku jumla ya watu 274,617 wakiripotiwa kupoteza maisha tangu janga la COVID-19 kuibuka nchini China mwishoni mwa mwaka jana. 

Marekani ndiyo inayoongoza kwa kuwa na vifo 77,180 pekee, ikifuatiwa na Uingereza yenye vifo 31, 241, Italia vifo 30,201, Uhispania vifo 26,478 na Ufaransa, ambayo imepoteza watu 26,230, kwa mujibu wa ripoti iliyokusanywa na shirika la habari la AFP, ambayo imetokana na vyanzo rasmi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Tatu Karema