1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaadhimisha siku ya Wafanyakazi

Lilian Mtono
1 Mei 2018

Leo ni siku ya kimataifa ya kuadhimisha mchango wa wafanyakazi kwenye maendeleo ya kijamii, kitaifa na kimataifa "Mei Mosi", ambapo kwa mara nyengine tena vilio vya wafanyakazi vimeendelea kusikia kote duniani.

https://p.dw.com/p/2wxTM
Indigene Völker und Umweltaktivisten auf den Philippinen versammeln sich vor der chinesischen Botschaft in Manila
Picha: DWA.P.Santos

Maelfu ya wafanyakazi pamoja na wanaharakati nchini Ufilipino wameandamana hii leo mjini Manila, wakipinga kile walichodai ni kushindwa kwa rais wa nchi hiyo, Rodrigo Duterte kutimiza ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni za urais ya kukabiliana na mikataba ya muda mfupi ya ajira.

Hata hivyo hakukua na ripoti yoyote ya machafuko, lakini makazi ya rais hapo awali yalifungwa ili kuwazuia waandishi wa habari kuingia kwenye eneo hilo, wakati waandamanaji walipochoma moto sanamu ya Duterte ikiwa ni ishara ya "Mfalme muongo" ambayo ilikuwa mita mia moja nje ya eneo hilo.

Ahadi ya kukabiliana na waajiri ambao huajiri wafanyakazi kwa mikataba ya muda mfupi na ambayo haikuwa na maslahi ya kutosha ilimsaidia Duterte, ambaye awali alikua meya wa jiji, kushinda urais katika uchaguzi wa Mei 2016.

Rodrigo Duterte
Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte, anashutumiwa na wafanyakazi kwa kushindwa kutekeleza ahadi yake.Picha: Getty Images/AFP

Makamu mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi cha Kilosang Mayo Un, KMU Lito Ustarez amesema wanakasirishwa na kutochukuliwa hatua yoyote na kuahidi kuendeleza mapambano hatua hadi serikali itakapokubaliana nao.

Muda mfupi baada ya kuingia madarakani, Duterte aliyaonya makampuni yaliyoshindwa kuondoa mikataba ya muda mfupi kuwa yanajiweka katika hatari ya kufungwa. Lakini vyama vya wafanyakazi vilisema hali hiyo imeendelea kujitokeza, hususani katika maduka makubwa ya bidhaa mchanganyiko na katika sekta ya maduka ya vyakula.

Pamoja na hatua kadhaa, lakini hali ya wafanyakazi haijabadilika nchini humo.

Kiongozi wa vuguvugu la mrengo wa kushoto la Bayan (Taifa), Renato Reyes, amesema rais Duterte amekifanya kile ambacho marais wengine walishindwa kukifanya katika kipindi cha miaka 30 cha kuunganisha makundi ya wafanyakazi yaliyokuwa yamegawanyika.

Akiwa kwenye mji wa Cebu, Duterte aliwaomba wabunge kupitisha marekebisho ya sheria ambayo alisema imepitwa na wakati na kuifanya kuwa ya kisasa inayokwenda na uhalisi wa wakati huu.

Kumekuwepo pia na maandamano kwenye miji mingine mikubwa nje ya mji mkuu wa Manila, ambapo vyama vya wafanyakazi vimedai kuongezwa kwa mishahara, kuboreshwa kwa mazingira ya ajira, ikiwa ni pamoja na mamilioni ya wafanyakazi wanaofanya kazi nje ya nchi.

Ufilipino imekuwa katika mzozo na Kuwait kufuatia ripoti za unyanyasaji dhidi ya wafanyakazi wa majumbani ambao ni raia wa nchi hiyo.

Ujerumani yakabiliwa na kitisho cha maandamano ya vurugu.

Mjini Berlin nchini Ujerumani, polisi zaidi ya 5,000 wamemwagwa mitaa mbalimbali ya mji huo ili kuhakikisha maandamano yanayofanywa na wafanyakazi na maadhimisho kwa ujumla yanakuwa ya amani.

1. Mai - Berlin - Demonstrationen der Gewerkschaften
Maandamano mjini Berlin mara zote huwa ya amaniPicha: picture-alliance/dpa/B. v. Jutrczenka

Wakati maandamano ambayo hufanywa na wafanyakazi katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya wafanyakazi mara nyingi yakifanyika kwa amani katika mji huo mkuu wa Ujerumani, eneo la Kreuzberg limekuwa likikabiliwa na migomo ya tangu Mei 1,1987, huku wafuasi wa mrengo mkali wa kushoto na waandamanaji walevi wakikabiliana na polisi.

Jumla ya maafisa wa polisi 5,300 kutoka kote Ujerumani wamekuwa wakipelekwa kukabiliana na visa vyovyote vya awali vinavyoashiria kutokea kwa machafuko. Ingawa maandamano hayo kiasi yamekuwa ya amani katika nyakati za hivi karibuni, bado kunatiliwa tahadhari kubwa kwa mwaka huu. 

Seneta wa wa mambo ya ndani wa Berlin, Andreas Geisel, mnamo siku ya Ijumaa alisema kuna uwezekano kuwa hali itakuwa mbaya kiasi kuliko mwaka jana.

Wachambuzi wanaamini kwamba wafuasi hao wa mrengo mkali wa kushoto wameungana zaidi mwaka huu, kwa kuangazia kampeni inayoendelea ya Uturuki dhidi ya Wakurdi waliopo kaskazini mwa Syria, ambao inasemekana wana ushawishi na maandamano hayo.

Mkuu wa polisi Barbara Slowik amesema polisi italazimika kutumia nguvu iwapo kutakuwepo na vitendo vyovyote vya uhalifu.    

Mjini Kuala Lumpur, waziri mkuu wa Malaysia Najib Razak ameahidi kuongeza kiwango cha chini cha mishahara mwaka huu iwapo atashinda kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Mei 9, akiongezea mrundikano wa ahadi kwa wapiga kura, katika wakati ambapo anakabiliwa na upinzani.

Najib amewaambia waandamanaji kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani kwamba ataongeza  kiwango cha chini cha mishahara kutoka kile cha sasa cha dola 255 kwa mwezi katika rasi ya Malaysia, lakini pia katika majimbo yaliyoko mashariki mwa nchi hiyo ya Sabbah na Sarawak, iwapo muungano wake utashinda. 

Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE/APE/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef