1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yalaani mashambulizi ya Nice

Mohammed Khelef15 Julai 2016

Viongozi duniani wameungana kulaani mashambulizi ya kigaidi nchini Ufaransa, ambayo yameangamiza maisha ya zaidi ya watu 80 waliokuwa wanangalia fashifashi kwenye mkesha wa siku ya kitaifa katika mji wa Nice.

https://p.dw.com/p/1JPIP
Nizza Polizei
Picha: picture-alliance/dpa/O.Anrigo

Nchini Ujerumani, jirani na mshirika wa Ufaransa kwenye masuala mengi ya kimataifa na Umoja wa Ulaya, Kansela Angela Merkel ameuita mkesha wa kuamkia Ijumaa (Julai 15) kuwa ni "wa kuhuzunisha", huku akiahidi kushirikiana na Ufaransa kwenye mapambano dhidi ya ugaidi. "Hakuna maneno yanayotosha kuelezea kile mshirika wetu, Ufaransa, anavyojihisi," alisema Kansela Merkel kwenye salamu zake za rambirambi.

Mashahidi wanasema watu kadhaa walilazimika kujirusha kwenye bahari kuyanusuru maisha yao, wakati mshambuliaji huyo alipoliendesha gari lake katikati ya watu waliokuwa wakiangalia maonesho ya fashifashi.

Rais Barack Obama wa Marekani ameyaita mashambulizi hayo kuwa ni ya kutisha, huku akisema kuwa nchi yake iko pamoja na Ufaransa, mshirika mkongwe kabisa katika historia. "Katika siku hii ya kitaifa kwa Ufaransa, tunakumbushwa kiwango cha juu kabisa cha ustahmilivu na maadili ya kidemokrasia yaliyoifanya nchi hiyo kuwa kigezo chema kwa ulimwengu mzima," alisema Obama.

Naye waziri wake wa mambo ya nje, John Kerry, ambaye yuko ziarani nchini Urusi, lakini ambaye alikuwepo Paris mchana wa jana (Alhamis ya Julai 14) kuhudhuria gwaride la siku hiyo ya kitaifa, alirejelea msimamo wa Rais Obama, huku akiita hii kuwa ni "siku ya huzuni" na kuahidi msaada wowote ambao Ufaransa ingeliuhitaji.

Urusi yaungana na ulimwengu kulaani mashambulizi

Akizungumza mjini Moscow kwenye mkutano wake na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, Kerry alisema mashambulizi ya Nice yanaongeza ulazima wa pande zote kushirikiana kuufyeka ugaidi.

Waombolezaji mjini Moscow wakiweka mashada ya maua kwenye ubalozi wa Ufaransa.
Waombolezaji mjini Moscow wakiweka mashada ya maua kwenye ubalozi wa Ufaransa.Picha: picture-alliance/dpa/TASS/S. Savostyanov

Urusi yenyewe imetoa tamko la kuyalaani mashambulizi hayo na pia kutangaza utayarifu wa kushirikiana na Ufaransa kwenye kipindi hiki kigumu. Msemaji wa ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov, amewaambia waandishi wa habari kuwa nchi yake "inachangiana hisia za kuondokewa na msiba pamoja na Ufaransa kutokana na vifo vya idadi hiyo kubwa ya watu, wakiwemo watoto."

Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter kwamba raia wa nchi yake wameshitushwa na mashambulizi hayo ya Nice. "Nyoyo zetu zi pamoja na wahanga, na mshikamano wetu na watu wote wa Ufaransa." Canada ina mahusiano ya kihistoria na Ufaransa, yenyewe ikiwa mchanganyiko baina ya jamii za Kifaransa na Kiingereza.

Borris: "Ni tukio la kuogofya"

Nchini Uingereza, jirani mwengine wa Ufaransa na mshirika wa kihistoria, msemaji wa Waziri Mkuu Theresa May, ameyaita mashambulizi hayo kuwa ni "tukio la kuogofya" akiongeza kwamba Uingereza imeshituka na kupatwa na wasiwasi. Waziri wake wa mambo ya nje, Boris Johnson, ambaye jukumu lake la kwanza lilikuwa kuhudhuria hafla ya Siku ya Kitaifa ya Ufaransa mjini London, alisema kwenye Twitter: "Nimeshitushwa na kuhuzunishwa na matukio ya kuogofya mjini Nice, na kupotea kwa maisha."

Polisi na kikosi cha zimamoto wakiwasili kwenye eneo la tukio muda mfupi baada ya kuanza kwa mashambulizi.
Polisi na kikosi cha zimamoto wakiwasili kwenye eneo la tukio muda mfupi baada ya kuanza kwa mashambulizi.Picha: Getty Images/AFP/V. Hache

Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk, aliita hiyo kuwa "ni siku ya msiba mkubwa kwa Ufaransa na kwa Ulaya nzima." Alisema lilikuwa jambo la "kuhuzunisha na baya zaidi watu walioshambuliwa walikuwa wakisherehekea uhuru, usawa na udugu."

Waziri Mkuu wa Uturuki, Binali Yildrim - ambaye mwenyewe nchi yake ni muhanga wa mashambulizi ya karibuni ya kigaidi kwenye uwanja wa ndege wa Istanbul - aliyalaani mashambulizi hayo ya Nice, akiyaita "mashambulizi ya watu woga yaliyomwagisha damu kwenye siku ya sherehe za kitaifa."

Kwa upande wake, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa umeyaita mashambulizi hayo kuwa yamefanywa na watu woga na makatili, huku Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang, akituma salamu za rambirambi akisema kuwa nchi yake inapingana na aina zote za ugaidi.

Ulimwengu wa Kiislamu walaani mashambulizi

Iran ni miongoni mwa mataifa ya karibuni kabisa yanayokaliwa na Waislamu wengi kupaza sauti yake dhidi ya mashambulizi hayo. Wizara ya Mambo ya Kigeni ya nchi hiyo imesema mashambulizi ya Nice yanadhihirisha haja ya kuwepo kwa ushirikiano madhubuti zaidi katika kupambana na ugaidi. Msemaji wa wizara hiyo, Bahram Ghasemi, ameongeza "ugaidi ni suala tata sana na linaweza tu kutokomezwa kwa mashirikiano na maridhiano ya kimataifa."

Katika barua yake maalum ya maombolezo kwa Rais Francoise Hollande wa Ufaransa, Rais Mahmoud Abbas wa Palestina ameyalaani mashambulizi hayo na kutangaza mshikamano wa Wapalestina na watu wa Ufaransa katika kipindi hiki kigumu. Ufaransa ni miongoni mwa mataifa ya Ulaya, ambayo yamekuwa na mtazamo unaoegemea Palestina katika mzozo wa Mashariki ya Kati.

Hasimu mkuu wa Palestina, taifa la Israel, nalo limepaza sauti yake kwenye msiba huu. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema mashambulizi haya ya Nice ni indhari kwamba ugaidi unaweza kushambulia popote, nao lazima upigwe vita popote pale ulipo.

Kauli kama hiyo imetolewa pia na makao makuu ya Kanisa Katoliki Duniani, Vatican, ambapo taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari inasomeka: "Tunalaani vikali aina zote za uovu, chuki, ugaidi na mashambulizi dhidi ya amani."

Afrika yaungana na ulimwengu

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.Picha: Tasnim

Huko Afrika Mashariki, ofisi ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya imechapisha tamko maalum kuhusu mashambulizi hayo, linalosema nchi hiyo inasimama na Ufaransa kwenye machungu ya msiba huu, huku pia ikiahidi kutoa ushirikiano wowote unaohitajika. Kama ilivyo Ufaransa, Kenya nayo ni muhanga wa mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi la al-Shabaab la Somalia.

Kaskazini mwa Afrika, Rais Abdel-Fattah al-Sissi wa Misri amemtumia salamu za rambirambi mwenzake wa Ufaransa, huku akiyaita mashambulizi hayo kuwa ni ugaidi wa kuchukiza kwenye mji wa Kifaransa". Naye Mufti Mkuu wa Misri, Shawki Allam, amesema mshambuliaji aliyeendesha gari lake kwenye umma wa watu amefuata njia ile ile ipitwayo na shetani, kwa kumwaga damu na kuwatendea maovu wale wasiokuwa na hatia.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amesema nchi yake inasimama pamoja na jumuiya ya kimataifa katika kulaani aina zote za ugaidi na inasimama na Ufaransa katika kuomboleza vifo vya raia wake.

"Ulaya inakabiliwa na vita"

Kwa ujumla, mashambulizi haya ambayo ni ya pili makubwa ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja ndani ya ardhi ya Ufaransa, yamedhihirisha kile wachambuzi wa masuala ya usalama wanachosema ni "urahisi" wa Ulaya kushambuliwa wakati wowote na mahala popote.

Waziri Mkuu wa Ubelgiji, yaliko makao makuu ya Umoja wa Ulaya na pia taifa ambalo limekuwa likichukuliwa kuwa kituo kikuu cha magaidi kupangia mashambulizi, Charles Michel, amesema hakuna suala kama "kutokuwepo kwenye hatari ya kushambuliwa na magaidi."

"Ukweli ni kuwa, sasa tunakabiliwa na namna mpya ya ugaidi," amesema katika wakati ambao nayo Ubelgiji inajitayarisha na sherehe zake za kitaifa wiki ijayo. Kama ilivyokuwa Ufaransa, Ubelgiji nayo bado imo kwenye kiwango cha juu cha hali ya tahadhari, ambapo vikosi vya wanajeshi na askari maalum wa kupambana na ugaidi vinaonekana kote mitaani.

Meya wa London, Sadiq Khan, amesema jiji hilo litahakiki upya mkakati wake wa ulinzi kwa sababu ya mashambulizi hayo ya Nice. Meya huyo amesema anataka kuhakikisha kuwa polisi wa London wanapewa vifaa na matayarisho ya kuushinda ugaidi. Kwa sasa, kiwango cha tathmini ya usalama inaiweka Uingereza kwenye nafasi ya juu, hiyo ikimaanisha kuwa nayo ina uwezekano mkubwa wa kuwa mlengwa wa mashambulizi ya kigaidi.

Bendera ya Ufaransa ikipepea nusu mlingoti kwa heshima ya wahanga wa mauaji ya Nice.
Bendera ya Ufaransa ikipepea nusu mlingoti kwa heshima ya wahanga wa mauaji ya Nice.Picha: Reuters/P. Wojazer
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya (kulia) na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya (kulia) na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.Picha: Reuters

Wakati huo huo, polisi nchini Ufaransa inasema imemtambua dereva wa gari lililouvamia umati wa watu katika mtaa wa Riviera mjini Niece, na kuwauwa 84 miongoni mwao.

Bila kumtaja jina, polisi inasema mwanamme huyo wa miaka 31 ambaye naye aliuawa na polisi, ni Mfaransa mwenye asili ya Tunisia. Taarifa hizo ni kutokana na nyaraka ambazo zimekutikana kwenye gari alilotumia kwenye mashambulizi hayo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/dpa
Mhariri: Daniel Gakuba