1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Duterte: Nitawachinja wahalifu wa madawa ya kulevya

Sylvia Mwehozi
30 Septemba 2016

Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amesema atakuwa mwenye furaha ikiwa "atawachinja"  watuhumiwa milioni tatu wa mihadarati. Ni matamshi makali zaidi aliyoyatoa katika vita vyake dhidi ya uhalifu.

https://p.dw.com/p/2QlHb
Philippinen Präsident  Rodrigo Duterte
Picha: picture-alliance/dpa/M.R.Cristino

Duterte ametoa kauli hiyo ya kitisho mapema hii leo Ijumaa wakati alipowasili katika mji wake wa nyumbani wa Davao, akitokea ziarani nchini Vietnam alikofanya majadiliano na viongozi wa nchi hiyo juu ya kampeni yake na namna serikali zao zinavyoweza kupambana na uhalifu wa kimataifa ikiwemo madawa ya kulevya.

Kiongozi huyo amesema vitisho vyake vya kifo dhidi ya washukiwa wa madawa ya kulevya vinalenga kuwatishia watuhumiwa kuacha biashara hiyo pamoja na kuwakatisha tamaa ambao wangependa kutumia. Lakini kauli zake za hivi karibuni zimepelekea mpango wake huo dhidi ya uhalifu katika kiwango kingine. "Hitler aliwachinja wayahudi milioni tatu. Kuna watuhumiwa milioni tatu wa madawa ya kulevya hapa, ndio wapo! Nitafurahi nikiwachinja wote. Angalau kama Ujerumani ilikuwa na Hitler, Ufilipino itakuwa na mimi, mnafafamu, wahanga wangu, ningependa niwamalize wahalifu wote, nimalize tatizo katika nchi na kukisaidia kizazi kijacho kutopotea" amesema rais Duterte.

Rais Barack Obama wa Marekani na Rodrigo Duterte wa Ufilipino
Rais Barack Obama wa Marekani na Rodrigo Duterte wa UfilipinoPicha: picture-alliance/dpa/N. Shrestha/M. Irham

Duterte anasema ikiwa wahanga wa Hitler walikuwa ni watu wasio na hatia, yeye anawalenga wahalifu wote. Hata hivyo ulinganisho wake na Hitler umekoselewa vikali na kaimu mkurugenzi wa shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch kwa Asia Phil Robertson anayesema kuwa. "Kiukweli Adolf hitler alikuwa ni miongoni mwa wauaji wakubwa katika historia ya binadamu, sasa kwanini mtu atake kujifananisha nae, hii inanishangaza. Lakini kama tungeiweka katika muktadha wa sasa Adolf Hitler angeshitakiwa kwa makosa dhidi ya ubinadam, angejikuta katika mahakama ya uhalifu wa kivita mjini the Hague. Ndicho anachokitaka Duterte? Je anataka kupelekwa katika mahakama hiyo? kwasababu naona anafanya kazi kuelekea huko".

Wakati wa kampeni zake za urais mapema mwaka huu na katika kipindi cha miezi mitatu akiwa madarakani rais huyo alitishia kuwazamisha watuhumiwa wote katika Ghuba ya Manila pamoja na kuwaua kwa kuwanyonga. Aliahidi kukomesha rushwa na uhalifu hasa madawa ya kulevya katika kipindi cha miezi sita madarakani. Na tangu ashinde uchaguzi mwezi Mei karibu watuhumiwa 3000 wa mihadarati wameuawa na karibu wengine 700,000 wamejisalimisha dhidi ya ukandamizaji wake lakini ameomba muda wa miezi sita zaidi ili kumaliza kazi yake.

Ndugu wakilia juu ya jeneza la mmoja wa watuhumiwa Ufilipino
Ndugu wakilia juu ya jeneza la mmoja wa watuhumiwa UfilipinoPicha: Getty Images/D. Tawatao

Wafuasi wake na raia wa Ufilipino ambao walikuwa wamechoshwa na kuenea kwa uhalifu wamepongeza hatua zake ngumu lakini amezidi kupata ukosoaji kutoka kwa jumuiya za kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Marekani wakisema ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Duterte amewaeleza wakosoaji wake hususan Umoja wa Ulaya kuwa ni "kundi la wapuuzi katika mfumo safi". Anasema Marekani ambayo ni mshirika wake wa siku nyingi na mataifa ya Ulaya yamekuwa na unafiki kwa kutowasaidia idadi kubwa ya wakimbizi wanaokimbia machafuko huko mashariki ya kati.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP

Mhariri: Iddi Ssessanga