1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DW na mimi, mimi na DW

23 Januari 2013

Uhusiano wangu na DW ulianzia mwaka 1987, nikiwa bado mwanafunzi huko visiwani Zanzibar, ambapo ilisaidia kunikuza sana kiakili licha ya kuwa bado na umri mdogo kabisa.

https://p.dw.com/p/17QH7
Der Journalist Mohamed Abdulahman. Januar, 2013, Bonn
50 Jahre Kisuaheli RedaktionPicha: DW

Uchambuzi wa matukio mbalimbali ya kisiasa, michezo na jamii ulinijengea shauku yangu kubwa na kuongeza maarifa na ujuzi katika kipindi changu cha kukuwa kiakili ni kimaarifa.

Niliweza kushiriki sana katika vipindi vya Barua na Salamu pamoja na Karibuni kwa kutuma salamu, maswali pamoja na hadithi fupi ambazo daima zilikuwa zikisomwa hewani mara kwa mara. Sisahau pia zawadi na bahashishi ambazo nilikuwa nikipokea kutoka DW.

Nazikumbuka vyema sauti nyororo za watangazaji wenu kama ile ya Maryam Hamdan, Kazungu Lozi na Oumilkheir Hamido. Sauti hizo zilikuwa zikivuma hewani kutangazia vipindi hivyo na vyenginevyo vinavyohusu jamii.

Namshukuru sana mkuu wa zamani wa Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle, Bwana Ben Wazir, kwa kutambuwa mchango wangu mkubwa wa kushiriki katika vipindi mbali mbali vya Idhaa hii na hatimaye kunipatia nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika kwa njia ya simu katika mijadala mbalimbali ya kisiasa hususani inayohusika na eneo hili la Mashariki ya Kati ambalo kwa hivi sasa ndipo nilipo kwenye kipindi cha Maoni Mbele Meza ya Duara.

Jambo hilo sio tu lilinisaidia sana kupata umashuhuri katika maeneo mbalimbali ambako matangazo DW yanasikika, lakini pia binafsi nimejifunza mengi kupitia washiriki wenzangu ambao miongoni mwao walikuwemo wasomi, wanasiasa, waandishi wa habari na wataalamu wa fani mbalimbali.

Kwa hakika katika kipindi hichi cha zaidi ya robo karne, ambayo ni nusu ya uhai wa Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle, nimeweza kunufaika, kujifunza na kuelimika kwa mambo mengi ambayo hadi hii leo yamekuwa yakinisaidia sana kimaisha na kimaarifa. Ni wazi, kwa hivyo, kwamba nitaendelea kuwa msikilizaji wenu wa kudumu na kushiriki katika matangazo yenu daima milele.

Tanbihi: Barua hii imeandikwa na Mbarouk Ghassany wa Muscat, Oman kwa ajili ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle.

Mhariri: Mohammed Khelef