1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EAC yatuma waangalizi wa uchaguzi Kenya

MjahidA18 Februari 2013

Jumuiya ya Afrika Mashariki imetuma kundi la waangalizi 40 watakaochunguza uchaguzi mkuu wa Kenya. Tayari wachunguzi 18 kutoka Muungano wa Ulaya waliwasili nchini humo mwishoni mwa Januari.

https://p.dw.com/p/17g4T
Wakenya katika chaguzi za zamani
Wakenya katika chaguzi za zamaniPicha: AFP/Getty Images

Kundi hilo la waangalizi kutoka nchi zote wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki isipokuwa Kenya, litaanza kazi yake hivi leo likiongozwa na aliyekuwa spika wa bunge la Afrika Mashariki Abdurrahman Kinana kutoka Tanzania.

Waangalizi hao wametoka taasisi mbali mbali zikiwemo Tume za Kitaifa za Haki za Binadamu, Bunge la Jumuia ya Afrika Mashariki, Tume za Uchaguzi za nchi wanachama, na waakilishi wa makundi ya vijana kutoka Jumuia ya Afrika Mashariki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kundi hilo mjini Nairobi, Katibu Mkuu wa Jumuia ya Afrika mashariki, Richard Sezibera amesema, amepata matumaini makubwa kutokana na hatua iliopigwa na serikali ya Kenya

Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

kuufanya uchaguzi mkuu ujao nchini humo, kuzingatia misingi ya maendeleo na uamuzi wa raia.

Sezibera pia amewatakia wakenya uchaguzi wa amani na Kenya mpya yenye uthabiti baada ya uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Machi 4 Mwaka huu. Tayari kundi la waangalizi 18 wa muda mrefu kutoka Muungano wa Ulaya wamo nchini Kenya kuanzia mwishoni mwa mwezi Januari na wataungana na wengine 18 watakaowasili tarehe 24 mwezi huu.

Serikali ya Kenya yapongezwa kwa maandalizi ya uchaguzi

Huku hayo yakiarifiwa nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashaiki zimeipongeza serikali ya Kenya kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao. Kwenye taarifa ya pamoja waliyoitoa baada ya kukutana na waziri wa Mashauri ya nchi za kigeni mjini Nairobi siku ya jumamosi, Waziri wa Mashauri ya nchi za Kigeni wa Uganda Sam Kutesa, Waziri wa Ulinzi wa Burunzi Gabriel Nizigama, Waziri wa Usalama wa Ndani nchini Burundi Sheikh Harerimama Musa Fazil na Waziri wa Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa nchini Tanzania Bernard Membe wamesisitiza haja ya kuzingatiwa kwa maoni ya wakenya ya kuchagua viongozi wanaowataka na kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa huru na wa haki.

Wakenya kuamua Machi 4
Wakenya kuamua Machi 4Picha: Roberto Schmidt/AFP/Getty Images

Mwandishi: Alfred Kiti

Mhariri: Josephat Charo