1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ebola, Boko Haram na Wakimbizi Magazetini

31 Julai 2014

Maradhi hatari ya Ebola, na mahojiano pamoja na mwandishi vitabu wa Nigeria, mshindi wa tuzo ya Nobel ya uandishi sanifu Wole Soyinka kuhusu Boko Haram ndizo mada zilizohanikiza magazetini wiki hii.

https://p.dw.com/p/1Cn28
Juhudi za kujikinga na maradhi ya kuambukiza ya Ebola nchini LiberiaPicha: picture-alliance/dpa

Tuanzie lakini Afrika magharibi ambako maradhi ya kuambukiza yanazidi kuangamiza maisha ya watu tangu mwezi february mwaka huu .Katika juhudi za kuepusha kuenea maradhi hayo,serikali ya Sierra Leone imetangaza hali ya hatari .Vikosi vya jeshi vinatumiwa kusafisha virusi vya Ebola majumbani.Na nchini Liberia nako serikali imeamua kuzifunga shule na kutangaza kuwaweka katika vituo vya uchunguzi wale wote walioambukizwa. Gazeti la Berliner Zeitung linazungumzia pia kitisho kwa watumishi wa mashirika ya misaada.Juhudi za kupambana na maradhi hayo zinakabiliwa na shida katika eneo la Afrika Magharibi hasa kwasababu wananchi wangali bado wanasumbuliwa na madhara ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika muda si mrefu uliopita nchini Liberia na Sierra Leone.Berliner Zeitung linazungumzia pia kadhia ya mgonjwa wa Ebola aliyefariki dunia Lagos, nchini Nigeria,nchi yenye wakaazi wengi zaidi barani Afria.Madhara ya kiuchumi yanayotokana na maradhi hayo ya Ebola yamemulikwa pia na Berliner Zeitung.Mashariki mengi ya kigeni yamewahamisha wafanyakazi wao kutoka Guinea ya Conacry,Sierra Leone na Liberia.Côte d'Ivoire nayo imefunga mipaka yake na Liberia,linamaliza kuandika gazeti hilo la mji mkuu.

Nguvu za kijeshi dhidi ya Boko Haram

Visa vya kikatili vinavyofanywa na wanamgambo wa itikadi kali wa Boko Haram tangu nchini Nigeria mpaka katika nchi jirani ya Cameroun ni miongoni mwa mada zilizomulikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika wiki hii.Gazeti la "die Tageszeitung" lilikuwa na mahojiano pamoja na mwandishi vitabu,mshindi wa tuzo ya uandishi sanifu ya Nobel Wole Soyinka kuhusu nini cha kufanya dhidi ya Boko Haram.Baada ya kuelezea huzuni na machungu kutokana na kutekwa nyara wanafunzi zaidi ya 200 ambao mbaka leo haijulikani kama kweli wako msituni,wako katika hali gani na kadhalika Wole Soyinka anazungumzia kichaa cha Boko Haram anaosema wanaitumia dini ili kuficha ukweli kwamba akili zao hazifayi kazi ipasavyo.Mshindi wa tuzo ya uandishi fasihi ya Nobel,Wole Soyinka anasema katika mahojiano hayo pamoja na gazeti la die Tageszeitung,ufumbuzi wa kijeshi ndio njia pekee ya kuwavunja nguvu Boko Haram.

Ulimwengu unapakata mikono

Gazeti la die Welt pia lilimulika visa vya Boko Haram."Hakuna anaefanya kitu isipokuwa Valérie" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti hilo inayozungumzia kampeni ya aliyekuwa mwandani wa rais wa Ufaransa Valérie Trierweller.Die Welt linasema mwandishi habari huyo ameanzisha kampeni yake kupigania wasichana zaidi ya 200 waliotekwa nyara na Boko Haram waachiliwe huru;anavaa kila siku fulana iliyoandikwa "Turejesheeni binti zetu".Hivi karibuni aliongoza maandamano pamoja na meya wa jiji la Paris Anne Hidalgo dhidi ya Boko Haram."Ni jukumu letu,kutowasahau" ameandika Valérie Trierweiler katika toleo lawiki hii jarida lake la "Paris Match".Anaamini ikiwa watu watakaa kimya basi wanasiasa hawatowajibika.

Die Welt linamalizia ripoti yake kwa kisa cha kutekwa nyara mke wa kaimu waziri mkuu wa Kamerun katika mji wa mpakani wa Kolofota.Watu wasiopungua 15 waliuwawa Boko Haram,walipoingia katika mji huo na kuivamia nyumba ya kaimu waziri mkuu Amadou Ali.

Magengi yajitajirisha kwa jasho la wakimbizi

Mada yetu ya mwisho katika makala hii ya Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inahusu ripoti ya gazeti la Neues Deutschland kuhusu fedha zinazowatoka wale wanaotaka kuingia Ulaya kinyume na sheria.

Neues Deutschland linasema kwa mara ya kwanza maafisa wa serikali nchini Hispania wamechapisha ripoti inayoonyesha magengi yanayowasafirisha wahamiaji kinyume na sheria wanawalazimisha wakimbizi wa Afrika wawalipe kati ya Euro 45 na Euro 6000,wakitaka kuingia katika nchin za Ulaya.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL PRESSE

Mhariri: Josephat Charo