1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ECOWAS kuongeza vikosi vyake Mali

27 Januari 2013

Mataifa ya Afrika Magharibi yamekubali kuongeza idadi ya wanajeshi wake watakaopelekwa Mali kuwaunga mkono wanajeshi wa nchi hiyo kupambana na waasi wenye itikadi kali za Kiislamu

https://p.dw.com/p/17SDa
Viongozi wa ECOWAS
Viongozi wa ECOWASPicha: picture-alliance/Landov

Uamuzi huo umefikiwa wakati ambapo vikosi vya Mali na Ufaransa vikidhibiti maeneo muhimu ya Gao. Viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi-ECOWAS waliokutana mjini Abidjan, Cote d'Ivoire wamefikia uamuzi huo ambapo sasa wanajeshi watakaopelekwa Mali watakuwa 7,700 badala ya 3,300 waliokubaliana awali. Mkuu wa Majeshi wa Cote d'Ivoire, Jenerali Soumaila Bakayoko amesema kuwa hadi sasa wanajeshi 1,750 kutoka nchi jirani za Afrika Magharibi wako Mali, huku Chad na Niger zikitoa wanajeshi 550 kila mmoja.

Hali ilivyo ndani ya Mali

Nchini Mali kwenyewe, vikosi vya Mali na Ufaransa vimefanikiwa kuudhibiti uwanja wa ndege na daraja muhimu katika mji wa Gao. Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian amesema kuwa wanajeshi hao wameudhibiti mji huo uliokuwa ukidhibitiwa na waasi tangu mwezi Juni mwaka uliopita na kwamba ngome kuu na magari ya waasi yameharibiwa. Msemaji wa jeshi la Ufaransa, Emmanuel Dosseur, amesema katika operesheni za kijeshi zinazoendelea eneo la Magharibi, wanajeshi walikuwa katika mji wa Lere uliopo umbali wa kilometa 440 kutoka Timbuktu. Watu walioshuhudia wamesema kuwa jeshi kubwa limeonekana katika mji wa Sevare uliopo umbali wa kilometa 570 kusini mwa mji wa Gao.

Wanajeshi wa Ufaransa walioko Mali
Wanajeshi wa Ufaransa walioko MaliPicha: Reuters

Uungaji mkono wa kimataifa

Wakati huo huo, Rais Barack Obama wa Marekani amekubali ombi la Rais Francois Hollande wa Ufaransa la kujaza mafuta ndege za kivita za Ufaransa ambazo zinaendesha operesheni dhidi ya waasi wa Mali. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, George Little amesema viongozi hao pia wamejadiliana kuhusu mipango ya Marekani kusafirisha wanajeshi kutoka mataifa ya Afrika katika jitihada za kuunga mkono juhudi za kimataifa katika suala la Mali. Aidha, Umoja wa Ulaya umesema jana kuwa utaanza kupeleka wakufunzi wa kijeshi ili kuwapatia mafunzo wanajeshi wa Mali katikati ya mwezi Februari huku wakufunzi wote 200 hadi 250 wakiwa Mali ifikapo katikati ya mwezi Machi. Ujerumani imegusia uwezekano wa kuiunga mkono Mali katika mkutano ujao wa wafadhili.

Mzozo wa Mali kutawala mkutano wa Umoja wa Afrika

Viongozi wa Umoja wa Afrika wanakutana leo mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambapo pamoja na mambo mengine wataujadili mzozo wa Mali, likiwemo suala la kupelekwa haraka kwa kikosi cha Afrika nchini humo. Kamishna wa Amani na Usalama wa umoja huo, Ramtane Lamamra, amesema kuwa nchi wanachama watapewa muda wa wiki moja kuandaa wanajeshi watakaopelekwa katika operesheni ya kijeshi nchini Mali chini ya vikosi vya kimataifa vitakavyoongozwa na Umoja wa Afrika-AFISMA. Umoja huo pia utaomba msaada wa muda wa kimkakati kutoka kwenye Umoja wa Mataifa kwa ajili ya AFISMA na kuuomba umoja huo kuidhinisha kuanzishwa haraka mipango ambayo itaiwezesha AFISMA kupeleka haraka wanajeshi wake na kupewa mamlaka ya kuendesha operesheni. Msaada wa kimkakati utajumuisha usafiri, madawa na hospitali katika maeneo ya mapambano.

Viongozi wa Umoja wa Afrika
Viongozi wa Umoja wa AfrikaPicha: picture-alliance/dpa

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,AFPE
Mhariri: Sekione Kitojo