1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ellen Johnson Sirleaf ashinda tuzo ya Mo Ibrahim

Iddi Ssessanga
12 Februari 2018

Rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, mshindi wa tuzo ya Nobel na mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa rais barani Afrika, ameshinda tuzo ya utawala bora ya Mo Ibrahim.

https://p.dw.com/p/2sY4q
Ellen Johnson-Sirleaf - ehemalige Präsidentin von Liberia
Picha: picture-alliance/dpa/EPA/EFE/J. Lizon

Tangu kuanza kwake, tuzo hiyo ilioasisiwa na tajiri wa mawasiliano raia wa Sudan Mo Ibrahim, imekosa mshindi mara kadhaa kwa sababu hakukuwa na watu waliotimiza vigezo.

Wakfu wa Mo Ibrahim umemsifu Johnson Sirleaf kwa uongozi wake wa kipekee wa mabadiliko, katika kusaidia kuifufua Liberia kutoka miaka kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Liberia ilioanzishwa na watumwa walioachiwa huru na Marekani, ndiyo jamhuri kongwe zaidi ya kisasa barani Afrika. Lakini imekumbwa na miaka kadhaa ya machafuko na umuagaji damu, ikiwemo vita viwili vya wenyewe kwa wenyewe vinavyokumbukwa kwa ukatili wake na matumizi ya watoto kama wanajeshi.

Mo-Ibrahim-Index für Regierungsführung in Afrika, 29.09.2014 in London
Mwasisi wa Tuzo ya utawala bora Afrika ya Mo Ibrahim, Mo Ibrahim kutoka Sudan.Picha: Barefoot Live

Johnson Sirleaf alichukuwa uongozi wa Liberia katika wakati ambapo ilikuwa inatafuta kuponya migawanyiko mikubwa na kujenga upya miundombinu yake.

Dhamira ya kufanikiwa

Utawala wake baada ya hapo ukakabiliwa na kuanguka kwa bei za bidhaa ulimwenguni, kulikoathiri sekta yake changa ya madini na kufuatiwa na mripuko mbaya wa ugonjwa wa Ebola. Licha ya changamoto hizo zote, Johnson Sirleaf alidhamiria kufanikiwa.

"Nina fursa ya kuwafungulia milango wanawake zaidi wa Kiafrika kushika nyadhifa ya juu za kisiasa, ni changamoto kwa sababu nawakilisha matarajio na matumaini ya wanawake wa Kiafrika wa Liberia, na pengine wanawake duniani na kwa hivyo shinikizo liko juu yangu kuhakikisha nafanikiwa."

Mwanzilishi wa tuzo hiyo Mo Ibrahim amesema katika mazingira magumu kabisaa Johnson Sirleaf aliisaidia nchi yake kuelekea mustakabali wa amani na kidemokrasia, na kumsafishia njia mrithi wake kufuata mkondo huo. Ameelezea matumaini kuwa Ellen Johnson Sirleaf ataendelea kuwahamasisha wanawake barani Afrika na kwingineko.

Salim Ahmed Salim amsifu Sirleaf

Tansania Salim Ahmed Salim
Mwenyekiti wa kamati ya tuzo ya Mo Ibrahim, Salim Ahmed Salim.Picha: DW/S. Khamis

Naye katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Afrika Salim Ahmed Salim, ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya tuzo hizo, amesema Sirleaf ameibadilisha Liberia, na kupelekea mchakato wa maridhiano uliojikita katika kujenga taifa na taasisi zake za demokrasia.

Katika kipindi chote cha mihula yake miwili, Salim amesema Johnson Sirleaf alifanya kazi bila kuchoka kwa niaba ya watu wa Liberia. Safari kama hiyo, amesema Salim, haiwezi kukosa kasoro, na mpaka sasa Liberia inaendelea kukabiliwa na changamoto kadhaa, lakini pamoja na hayo, Johnson Sirleaf ameweka msingi ambako Liberia inaweza kujengea, amesema Salim Ahmed Salim, ambaye pia ni waziri mkuu wa zamani wa Tanzania.

Washindi wa awali wa tuzo hiyo ni pamoja na Joaquim Chissano wa Msumbiji, alieshinda mwaka 2007, Festus Mogae wa Botswana mwaka 2008, Pedro Pires wa Cape Verde mwaka 2011, na Hifikepunye Pohamba wa Namibia mwaka 2014. Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela alifanywa mshindi wa heshima wa tuzo hiyo mwaka 2007.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre.

Mhariri: Mohammed Khelef