1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan aahidi hatua kali dhidi ya "wasaliti"

Sekione Kitojo
16 Julai 2017

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ameapa kuchukua hatua kali dhidi ya wanaodaiwa kushiriki jaribio la mapinduzi mwaka mmoja uliopita, akisisitiza kuomba kurejeshwa kwa adhabu ya kifo dhidi ya wale anaowaita wasaliti.

https://p.dw.com/p/2gcBV
Istanbul Jahrestag Putschversuch Erdogan Rede
Picha: Reuters/Turkish Presidency

Akizungumza mbele ya umati wa watu waliohudhuria kumbukumbu za mwaka mmoja za jaribio hilo jana Jumamosi (15 Julai) katika daraja mjini Istanbul, Erdogan alisema: "Wale wasaliti watakumbukwa daima kwa  kuchukiwa," akiongeza kwamba  Uturuki "haijawahi kusita kuvunjavunja vichwa vya wale wanaosaliti."

Pia ameahidi "kuwakata vichwa wasaliti kwanza," akimaanisha  magaidi, katika hotuba ambayo iliambatana na rejea za  maandiko ya Kiislamu na ukosoaji mkubwa dhidi ya upinzani.

Istanbul Bosporus Brücke Jahrestag Putschversuch
Umati wa watu waliohudhuria maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kufanyika jaribio la mapinduzi nchini UturukiPicha: Getty Images/AFP/Y. Akgul

Erdogan aliongeza kwamba wafungwa waliokamatwa kwa kuhusika na jaribio la mapinduzi sasa wanavaa "sare zinazofanana  na Guantanamo mahakamani, akimaanisha  gereza lenye utata la Marekani nchini Cuba.

Hotuba hiyo katika daraja la Bosporus, ambalo lilipewa jina jipya  la daraja la mashahidi mwaka jana na lilikuwa moja ya  sehemu za mapaigano katika jaribio la mapinduzi mwaka 2016, yaliyofanyika mbele ya maelfu ya watu waliokuwa  wakipepea bendera ya Uturuki.

Türkei | 1. Jahrestag des Putschversuches
Sehemu ya wananchi wanaohudhuria maadhimisho ya mwaka mmoja baada ya jaribio la mapinduzi nchini Uturuki katika daraja maarufu la BosporusPicha: Getty Images/C. McGrath

Erdogan pia alishiriki katika maadhimisho ya usiku wa manane mjini Ankara kwa wale waliofariki katika jaribio hilo la  mapinduzi, wakati wabunge wa upinzani walisusia tukio hilo.

Upinzani waishutumu serikali

Hapo mapema siku ya Jumamosi katika mji mkuu, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Uturuki alishutumu  kushindwa kwa serikali kuzuwia jaribio la mwaka jana la mapinduzi na hali inayoendelea ya kukamatwa kwa wale wanaodaiwa kuunga mkono mapinduzi wakati wa kikao maalum cha bunge kuadhimisha mwaka mmoja tangu kusjhindwa kwa jaribio hilo la mapinduzi.

Türkei Jahrestag Putschversuch Erdogan- Puppe von Fethullah Gulen als Häftling
Taswira ya mwanasesere inayowakilisha Fethullah Gulen ikining'inia kama ishara ya kutaka aadhibiwePicha: Getty Images/C. McGrath

Kemal Kilicdaroglu, kiongozi wa chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha People's Republican Party (CHP) aliwashutumu viongozi wa serikali kwa kudai kwamba maafisa ambao waliruhusu waliokula njama ya mapinduzi "kujipenyeza  katika maeneo nyeti ya serikali" wawajibishwe.

Serikali inamlaumu imamu anayeishi uhamishoni nchini Marekani, Fethullah Gulen, kwa kuhusika na jaribio hilo la mapinduzi  la Julai 15, ambaye aliwahi kuwa mshirika mkubwa wa chama tawala cha Justice and Development (AKP).

Wafuasi wa Gulen walidaiwa kuweza kujipenyeza katika utaratibu wa utawala na jeshi na kufanya jaribio hilo lililoshindwa, lakini  Gulen amekana kuhusika na jaribio hilo.

Türkei Jahrestag Putschversuch
Maelfu ya watu waliojitokeza kuunga mkono maadhimisho hayo mjini IstanbulPicha: Reuters

Maswali mengi yanaendelea kubaki juu ya jaribio hilo, ikiwa ni pamoja na kutambua nani hasa anahusika na lini serikali ilifahamu njama hizo. Baadhi ya maafisa wa jeshi wanaoshutumiwa kuwa ni wapangaji wa jaribio hilo wanakana kuwa na mahusiano na Gulen.

Serikali imeitangaza  tarehe 15 Julai kuwa sikukuu ya kitaifa ya "demokrasia na umoja" kwa kulieleza jaribio lililoshindwa  kuwa  ni ushindi wa kihistoria kwa demokrasia nchini Uturuki.

Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe/dpae

Mhariri: Mohammed Khelef