1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan akamilisha ziara yake ya Ujerumani

Bruce Amani
30 Septemba 2018

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan amekamilisha ziara yake ya siku tatu nchini Ujerumani, akisema kuwa ziara hiyo yenye utata imekuwa yenye mafanikio makubwa. Mamia ya watu, wakiwemo Wakurdi walijitokeza Cologone

https://p.dw.com/p/35iqS
Deutschland Türkischer Präsident Erdogan in Köln
Picha: picture-alliance/dpa/H. Kaiser

Amesema anaamini mikutano iliyofanyika kwa siku mbili imeimarisha urafiki wa muda mrefu kati ya Ujerumani na Uturuki na kwamba nchi hizo zinahitaji kuzingatia maslahi ya pamoja na kuziacha tofauti zilizojitokeza hivi karibuni. Erdogan aliikamilisha ziara yake mjini Cologne ambapo aliufungua mmoja wa misikiti mikubwa barani Ulaya.

Msikiti huo mpya unaendeshwa na jumuiya ya Waislamu wa Uturuki wanaoishi Ujerumani, DITIB. Baada ya kuwasili Cologne, Erdogan alikutana na Waziri Mkuu wa jimbo la North-Rhine Westphalia, Armin Laschet. Erdogan ameitaka Ujerumani kukabiliana vikali na wapiganaji wa Kikurdi. Pia amesema mchezaji maarufu wa mpira wa miguu, Mesut Özil alilazimika kustaafu kuichezea timu ya taifa ya Ujerumani kutokana na asili yake ya Uturuki.

Wakati wa hotuba yake, Erdogan pia alitoa wito wa kujumuishwa katika jamii watu milioni tatu wa asili ya Uturuki wanaoishi Ujerumani na akatoa wito wa kuanzishwa uraia wa nchi mbili

Deutschland Zentralmoschee-Einweihung in Köln l Erdogan-Anhänger
Wafuasi wa Erdogan walijitokeza ColognePicha: Getty Images/C. Koall

Akiwa Cologne, rais huyo wa Uturuki alisema Fethullah Gulen, mhubiri wa Uturuki anayeishi Marekani ambaye anatuhumiwa kwa jaribio lililoshindwa la mapinduzi ya kijeshi Julai 2016, na wafuasi wake hawapaswi kupewa hifadhi Ulaya.

Polisi mjini Cologne ilifanya mojawapo ya operesheni kali kabisa katika historia yake ili kuhakikisha ulinzi wakati wa ziara hiyo.

Akizungumza baada ya kukutana na kiongozi huyo wa Uturuki, waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westphalia Armin Laschet amesema mahusiano kati ya Ujerumani na Uturuki yanagubikwa na wasiwasi kuhusu utawala wa sheria na lazima hayo yashughulikiwe kama Erdogan anataka kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na Ujerumani.

Wasiwasi wa usalama na tofauti za kisiasa vililazimisha kufanyika mabadiliko ya dakika za mwisho mwisho kwa ratiba ya Jumamosi ya Erdogan.

Mkutano kati ya Erdogan na Laschet ulipangwa upya ili kufanyika katika uwanja wa ndege wa Cologne/Bonn baada ya mkutano uliopangwa awali katika jumba la kale la Wahn kufutwa kwa sababu mmiliki wa ngome hiyo alisema Erdogan hakaribishwi kutokana na sababu za kisiasa.

Mipango ya kuandaa mkutano mkubwa wa wazi katika eneo la msikiti uliozinduliwa rasmi ilifutwa Ijumaa na mamlaka za mji wa Cologne kwa sababu za kiusalama.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Grace Patricia Kabogo