1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan arejea nyumbani, maandamano yaendelea

7 Juni 2013

Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amerejea nchini mwake kutoka ziarani Afrika ya Kaskazini, na kutoa wito wa kusimamishwa mara moja kwa maandamano ambayo yameendelea nchini mwake kwa siku saba mfululizo.

https://p.dw.com/p/18lXu
Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amerejea nyumbani na kulakiwa na maelfu
Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amerejea nyumbani na kulakiwa na maelfuPicha: Reuters

Alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Istanbul usiku wa kuamkia leo, Recep Tayyip Erdogan alilakiwa na umati wa wafuasi wa chama chake cha Haki na Maendeleo, AKP, waliopeperusha bendera ya uturuki, na kupaza sauti wakimuahidi kuwa tayari kufa kwa ajili yake, huku wakitishia kwenda kuwatawanya watu wanaoandamana kumpinga. Akiwahutubia watu hao, Erdogan aliwasifia kwa kubakia watulivu muda huu wote, na kuonyesha umakini na ukomavu, na kisha kuwataka waende nyumbani.

Kabla ya kuwasili kwake, maelfu ya waandamanaji wanaoipinga serikali yake waliingia katika mitaa ya miji mbali mbali ya Uturuki, wakikariri wito kumtaka Erdogan ajiuzulu. Jibu lake alipowasili nchini lilikuwa la ukaidi.

Uwanjani Erdogan alilakiwa na maelfu ya wafuasi wake
Uwanjani Erdogan alilakiwa na maelfu ya wafuasi wakePicha: Getty Images

''Natoa wito kwa maandamano haya kusitishwa mara moja, kwa sababu yamepoteza uhalali wa kidemokrasia, na sasa yamegeuka fujo'. Alisema Erdogan.

Njia pekee ni uchaguzi

Erdogan alisema aliingia mardarakani kupitia njia ya uchaguzi, na kuapa kuwa njia pekee ambayo ataachia madaraka ni hiyo hiyo ya visanduku vya kura. ''Hatuwezi kumfumbia macho mtu yeyote atakayeyumbisha amani ya nchi, na kujaribu kuiteka nyara demokrasia'', alionya waziri mkuu huyo.

Erdogan alisema miongoni mwa waandamanaji wapo watu wanaohusishwa na visa vya ugaidi, na kuongeza kuwa watu saba wasio waturuki wamekamatwa katika maandamano hayo, bila kutoa maelezo zaidi.

Akizungumza nchini Tunisia jana, waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan alishikilia msimamo wake kuwa mradi wa ujenzi wa duka kubwa katika bustani ya mjini Istanbul utaendelea kama ulivyopangwa, akisema ulinzi wa mazingira hauhusishi tu masuala ya miti, bali pia yale ya kitamaduni.

Ukaidi wazidi kuchochea hasira

Ukaidi wa Recep Tayyip Erdogan haukuwapendeza wengi wa waandamanaji hao, ambao walitegemea kusikia wito wa maridhiano kutoka kwake.

Maelfu ya wapinzani wa waziri mkuu wa Uturuki nao wameendelea kuandamana.
Maelfu ya wapinzani wa waziri mkuu wa Uturuki nao wameendelea kuandamana.Picha: Reuters

''Watu hawakupendezwa na kauli yake ya hivi karibuni, watu hawa wamekuwa wakikusanyika hapa kwa wiki nzima, na walitegemea aombe radhi, lakini hawakusikia kitu kama hicho.'' Alisema mwandamanaji mmoja.

Mwandamanaji mwingine alisema kuwa kilichoanza kama harakati za kutetea mazingira, kinageuka sasa mapambano ya kutetea uhuru.

Waliokufa sasa ni 3

Vyombo vya habari nchini Uturuki vimeripoti kifo cha mtu wa tatu kutokana na maandamano hayo, dhidi ya kile ambacho waandamanaji wanakiita mwelekeo wa waziri wao mkuu kuzidi kuitawala nchi kiimla.

Taarifa kutoka hospitalini zimeelezea kuwepo kwa maelfu ya watu waliojeruhiwa, wakati polisi ikijaribu kuwatawanya ikitumia mabomu ya kutoa machozi, na mizinga ya maji.

Racep Tayyip Erdogan ameshinda uchaguzi mara tatu nchini mwake, licha ya kukabiliwa na upinzani mkubwa kisiasa. Mbali na kulalamikia utawala wa waziri mkuu huyo wanaouita wa kiimla, waandamanaji pia wanapinga mpango wa kuanzishwa sheria kali zinazodhibiti uhuru wao, ikiwemo ile inayoweka kiwango cha kileo ambacho watu wanapaswa kunywa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/DPAE

Mhariri:Josephat Charo