1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan asema Macron anahitajia matibabu

Iddi Ssessanga
24 Oktoba 2020

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan amemshambulia mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron Jumamosi, akisema anahitaji matibabu ya akili kuhusiana na mtazamo wake kwa Waislamu na Uislamu.

https://p.dw.com/p/3kO76
Frankreich Paris | Staatstreffen | Erdogan und Macron
Picha: picture-alliance/AP Photo/L. Marin

Mapema mwezi huu, Macron aliapa kupambana dhidi ya kile alichokiita kujitenga kwa wafuasi wa itikadi kali ya Uislamu, ambako alisema kunatishia kuchukua udhibiti wa baadhi ya jamii za Waislamu nchini Ufaransa, hatua iliyokaripiwa vikali na Erdogan.

Ufaransa ilitikisa na kukatwa kichwa kwa mwalimu wa historia na mfuasi wa itikadi kali, alietafuta kulipiza kisasi kwa hatua ya mwalimu huyo kutumia vibonzo vya Mtume Muhammad katika darasa lake la uhuru wa kujieleza.

Soma pia: Macron aiomba Ulaya kuikemea Uturuki

"Ni nini tatizo la huyu mtu anaeitwa Macron na Uislamu na Waislamu? Macron anahitaji matibabu kwa ngazi ya akili," Erdogan alisema katika hotuba kwa mkutano wa mkoa wa chama chake cha AKP katika mji wa katikati mwa Uturuki wa Kayseri.

"Nini kingine kinaweza kusemwa kwa mkuu wa nchi asieelewa uhuru wa imani na mwenye tabia ya namna hii kwa mamilioni ya watu wanaoishi nchini mwake, ambao ni waumini wa dini tofauti?" Erdogan aliongeza.

Frankreich | Paris | Macron bei der Gedenkzeremonie für den Lehrer Samuel Paty 21.10.2020
Rais Emmanuel Macron ameuelezea Uislamu kama dini iliyoko katika mzozo kote duniani, hatua iliyoikasirisha serikali mjini Ankara.Picha: Francois Mori/Pool/Reuters

Erdogan ni Muislamu mcha Mungu na tangu chama chake cha AKP chenye misingi yake ya Kiislamu kuingia madarakani mwaka 2002, ametafuta kuufanya Uislamu kuwa sehemu ya siasa kuu nchini Uturuki, taifa lenye idadi kubwa sana ya Waislamu lakini lililokuwa linafuata misingi ya kilimwengu.

Soma pia: Uturuki yatuhumu 'hatua za ubabe'' za Ufaransa

Rais huyo wa Uturuki alisema Oktoba 6 baada ya matamshi ya kwanza ya Macron kuhusu "Uislamu wa kujitenga", kwamba matmshi hayo ni "uchokozi wa wazi" na yalionyesha ufidhuli wa kiongozi huyo wa Ufaransa.

Uturuki na Ufaransa ni wanachama wa jumuiya ya NATO lakini zimekuwa katika malumbano juu ya masuala kadhaa, yakiwemo sera nchini Syria na Libya, mipaka ya baharini mashariki mwa Mediterania na mzozo katika jimbo la Nagorno-Karabakh.

Erdogan na Macron walijadili tofauti zao katika mazungumzo ya simu mwezi uliyopita, na walikubaliana kuboresha uhusiano na kuweka wazi njia za mawasiliano.