1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan ashinda kura ya maoni, wapinzani walalamika

Sekione Kitojo
17 Aprili 2017

Rais wa Uturuki Erdogan ameibuka mshindi katika kura ya maoni ya kihistoria itakayoimarisha madaraka yake. Matokeo yameiacha nchi ikigawanyika mno na upinzani unasema upigaji kura haukukuenda sawa.

https://p.dw.com/p/2bKan
Türkei Referendum Wahllokal in Istanbul Präsident Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan Picha: Reuters/A. Konstantinidis

Mabadiliko  hayo  makubwa  ya  katiba  yaliyoidhinishwa  kupitia kura  hiyo  ya  maoni yanaunda  mfumo  wa  madaraka  ya  rais ambao  utampa  rais Erdogan  madaraka  zaidi  kuliko  kiongozi yeyote  tangu  muasisi  wa  Uturuki Mustafa Kemal Ataturk  na mrithi wake  Ismet Inonu.

Kambi  ya "ndio" imeshinda  kwa  asilimia  51.4 ya  kura  dhidi  ya asilimia  48.6 kwa  upande  wa  "hapana", tume  ya  uchaguzi imesema  katika  tarakimu  zilizonukuliwa  na  shirika  la  habari  la Anadolu, katika  zoezi  la  kuhesabu  kura  kwa  misingi  ya  asilimia 99.5 ya  masanduku  ya  kura. Watu waliojitokeza  kupiga  kura  ni asilimia  85.

Türkei Regierung erklärt Sieg bei Referendum
Watu wakipunga bendera wakifurahia ushindi wa ErdoganPicha: picture alliance/AA/H. Yaman

Matokeo  ya  kura  hiyo  pia  yanaathari  pana  kwa  Uturuki  ambayo imejiunga  na  jumuiya  ya  kujihami  ya  NATO mwaka  1952 na katika  kipindi  cha  mwisho  cha  nusu  karne  nchi  hiyo  imelenga katika  kujiunga  na  Umoja  wa  Ulaya.

Sherehe mitaani

Kundi  kubwa  la  watu  waliokuwa  wakipunga  bendera walisherehekea  ushindi  huo  mitaani, Erdogan  akiisifu  Uturuki kwa kuchukua "uamuzi  wa  kihistoria".

Türkei Referendum |  Abstimmung
Mifuko ya kura kutoka katika vituo vya kupigia kura nchini UtrukiPicha: picture alliance/AA/E. Atalay

"Pamoja  na  umma, tumeweza  kufikia  mabadiliko  muhimu  katika historia  yetu," ameongeza.

Lakini  waungaji  mkono  wa upinzani  katika  wilaya  zinazompinga Erdogan  za  mjini  Istanbul  wameonesha  kutoridhishwa  kwa kupiga mabakuli  na  sufuria kwa  vijiko  na  umma  na  kufanya kelele  za  kupinga. Mamia  ya  watu  pia  waliingia  mitaani  katika maeneo  ya  Besiktas  na  Kadikoy.

Mkuu  wa  mamlaka  kuu  ya  uchaguzi  Sadi Guven  amethibitisha kwamba  kambi  ya  "ndio" imeibuka  mshindi, lakini  upinzani umeapa  kupinga  matokeo  hayo.

Kura  hiyo  ya  maoni  ilifanyika  chini  ya  amri  ya  hali  ya  hatari ambayo  imeshuhudia  watu  47,000 wakikamatwa  katika ukandamizaji  baada  ya  jaribio  lililoshindwa  la  mapinduzi  dhidi  ya Erdogan Julai  mwaka  jana.

Türkei Yildirim verkündet den Sieg der Ja-Sager
Waziri mkuu wa Uturuki na kiongozi wa chama tawala cha AKP Binali YildirimPicha: picture alliance/AA/A. Balikci

Mwishoni  mwa  kampeni iliyokuwa  na  hamasa  nyingi , kambi  ya "hapana" iliweza  kuongeza  idadi  ya  kura  wakati  kura  zaidi zikihesabiwa , baada  ya  kuwa  nyuma  kwa  muda  mrefu  katika matokeo  ya  awali, lakini  kambi  hiyo  ilishindwa  kuipita  kambi  ya kura  za  "ndio".

Wakati  huo  huo theluthi  mbili  ya  Waturuki  wanaoishi  nchini Ujerumani wamepiga  kura  zao  wakimuunga  mkono  rais Recep Tayyip Erdogan katika  kura  ya  maoni  inayotaka  kumpa  madaraka zaidi  rais. Asilimia  63.1  ya  wapigakura  Waturuki  nchini Ujerumani  wameunga  mkono  hatua  hiyo, limesema  shirika  la habari  la  Uturuki Anadolu  mapema  leo  Jumatatu.

Brexit-Hauptakteure - Jean-Claude Juncker
Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude JunckerPicha: Getty Images/C. Court

Maoni ya viongozi mbali mbali

Taarifa ya  pamoja ya rais  wa  Halmashauri  ya  Umoja  wa  Ulaya Jean-Calude Juncker  na  waziri  mwenye  dhamana  ya  masuala ya  kigeni  katika  Umoja  huo  Federica Mogherini  imesema , mabadiliko  ya  katiba  na  hususan utekelezaji  wake utatathminiwa kwa  misingi  ya  jukumu  la  Uturuki  kama nchi  inayotaka  kujiunga na  Umoja  huo  na  mwanachama  wa  baraza  la  Ulaya.

Mkuu  wa  jukwaa  la  haki  za  binadamu  barani  Ulaya Thorbjorn Jagland  amesema  kwamba  Uturuki  inapaswa  kupima  hatua  yake nyingine  kwa makini  baada  ya  kura  hiyo  ya  maoni ambapo kambi  ya "ndio" ilishinda  kwa  kiwango  kidogo.

Mwandishi: Sekione Kitojo /dpae / afpe

Mhariri: Yusra Buwayhid