1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan: Huenda tukarejesha adhabu ya kifo

Mohammed Khelef19 Julai 2016

Katika kile kinachoonekana kuwa operesheni ya aina yake baada ya kushindwa jaribio la kumpindua Rais Recep Tayyip Erdogan, serikali ya Uturuki imewafukuza kazi maafisa 9,000, huku ikiwafikisha mahakamani majenerali 26.

https://p.dw.com/p/1JREh
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki (kulia) na mpinzani wake mkuu, Fethullah Gulen, anayemtuhumu kutaka kumpindua.
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki (kulia) na mpinzani wake mkuu, Fethullah Gulen, anayemtuhumu kutaka kumpindua.Picha: picture-alliance/Zaman/AA/B. Ozkan

Hali nchini Uturuki kwa sasa ni mkorogovyogo, licha ya jeshi kutangaza rasmi hapo jana kwamba wameshaidhibiti hali na jaribio hilo la mapinduzi limezimwa moja kwa moja. Waziri Mkuu Binali Yildrim anasema zaidi ya watu 7,500 wamewekwa kizuizini, wakiwemo majenerali na maadmirali 103.

Wizara ya mambo ya ndani inasema takribani watu 9,000, kati yao maafisa wa polisi 8,000 na pia magavana wa mabaraza ya miji, wamefutwa kazi kwenye fagiafagia inayoendelea. Wafanyakazi wote wa sekta ya umma wamezuiwa kuchukuwa likizo zao hadi hapo mchujo utakapomalizika.

Hii ni katika utekelezaji wa kile Rais Erdogan anachokiita "kusafisha virusi" vilivyomo kwenye vyombo vya dola na sekta ya umma.

Serikali inamshutumu rafiki wa zamani wa Erdogan na hasimu wake mkubwa wa sasa, Fethullah Gulen, ambaye anaishi uhamishoni nchini Marekani kwa kuhusika na jaribio hilo la mapinduzi.

Kiongozi huyo wa kidini ana ufuasi mkubwa miongoni mwa maafisa kadhaa wa serikali ya Erdogan, kuanzia mahakama, hadi polisi na mabaraza ya miji, ingawa hana ushawishi wa kutosha jeshini. Mwenyewe anakanusha kuhusika kwa namna yoyote na jaribio hilo, ambalo limeangamiza maisha ya watu wapatao 300, huku 100 kati yao wakiwa wanajeshi walioasi.

Erdogan ataka kurejesha adhabu ya kifo

Akizungumza na wafuasi wake mjini Istanbul, Rais Erdogan amesema upo uwezekano wa kurejeshwa kwa adhabu ya kifo, ili kuwatia adabu wale waliohusika na jaribio hilo, huku akiwalaumu wale wote wanaojitokeza kuwatetea ama kuwahurumia.

Maafisa wa kijeshi wakiendelea kutiwa nguvuni kwa tuhuma za kushiriki jaribio la mapinduzi la tarehe 15 Julai 2016 nchini Uturuki.
Maafisa wa kijeshi wakiendelea kutiwa nguvuni kwa tuhuma za kushiriki jaribio la mapinduzi la tarehe 15 Julai 2016 nchini Uturuki.Picha: picture-alliance/abaca/T. Adanali

"Wale wanaojaribu kuanzisha daraja la mafahamiano kati ya mahaini na taifa ni magaidi wao wenyewe. Kwa sababu hakuna mafahamiano kama hayo. Jaribio hili ni uhaini kwa nchi hii, na wataadhibiwa ipasavyo. Wataadhibiwa kwa namna ile ile ambayo uhaini huadhibiwa kwengineko duniani."

Hayo yanatokea huku wito ukizidi kuongezeka kutoka kwa washirika wa Kimagharibi, kuitaka Uturuki isirejeshe hukumu ya kifo. Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa na Marekani, zimepaza sauti zao kumuonya kwa kutumia hatua za kikandamizaji dhidi ya washukiwa hao.

Msemaji wa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Steffan Siebert, amelaani vikali matukio ya kuogofya na visasi, yakiwemo ya kufukuzwa kazi majaji zaidi ya 2,000 kwa wakati mmoja na pia mateso dhidi ya wanajeshi mitaani wanaoshukiwa kushiriki jaribio hilo.

"Suala hili linazusha masuala na wasiwasi mkubwa, pale unapokuta kuwa siku moja tu baada ya jaribio la mapinduzi, majaji 2,500 wanaondoshwa kwenye nafasi zao. Kila mmoja anaelewa kuwa dola na mahakama za Uturuki zinapaswa kuchukuwa hatua dhidi ya waliohusika na jaribio hilo, lakini utawala wa kisheria lazima nao udumishwe," alisema Siebert.

Hapo jana, aliyekuwa mkuu wa kikosi cha anga, Jenerali Akin Ozturk, alikuwa mmoja wa majenerali 26 waliopandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza, na kusomewa mashitaka ya kula njama za kufanya mapinduzi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/afpe,rtre
Mhariri: Daniel Gakuba