1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan rais mteule Uturuki, ataka maridhiano

11 Agosti 2014

Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameahidi mwanzo mpya, baada ya kupata ushindi mwepesi katika uchaguzi wa rais uliofanyika Jumapili, licha ya hofu kuwa nchi hiyo ilikuwa inaelekea kwenye utawala wa mtu mmoja.

https://p.dw.com/p/1CsIa
Präsidentschaftswahl in der Türkei Erdogan 10.08.2014
Picha: REUTERS

Waziri mkuu Erdogan alishinda asilimia 52 ya kura, na kumuacha mbali kabisa mpinzani wake wa karibu Ekmeleddin Ihsanoglu, aliepata asilimia 38, huku mshindi wa tatu, Mkurdi Selahattin Demirtas akipata asilimia 9.7 ya kura. Matokeo hayo yalikuwa ushindi binafsi wa Erdogan mwenye umri wa miaka 60, ambaye amehudumu kama waziri mkuu tangu mwaka 2003, na huenda akawa rais kwa mihula miwili hadi mwaka 2024.

Maelfu ya wafuasi walifurika katikati mwa mji wa Istanbul wakipeperusha bendera za Uturuki na kubeba picha za Erdogan kusherehekea ushindi, huku fataki zikitanda katika anga ya mji mkuu Ankara. Akiwahutubia maelfu waliokuwa wakimsikiliza katika makao makuu ya chama chake cha AKP mjini Istanbul, Erdogan alisema ni wakati wa kuanza enzi mpya.

Wafuasi wa Erdogan wakisherehekea ushindi mjini Istanbul.
Wafuasi wa Erdogan wakisherehekea ushindi mjini Istanbul.Picha: REUTERS

"Ndugu zangu, nayasema haya kutoka moyoni. Naomba tuanze kipindi kipya cha maridhiano ya kijamii leo, na tuache majadiliano ya zamani katika Uturuki ya zamani. Tuache malumbano, utamaduni wa makabaliano na matatizo mengine katika Uturuki ya zamani," alisema Erdogan huku akishangiliwa na wafuasi wake.

Wito kwa wapinzani

Erdogan pia aliwatolea wito wapinzani wanaomuita dikteta kujiuliza badala ya kumkosoa. Alisema upinzani wa kisiasa unapaswa kurejea sera zake ili kuendana na wazo la Uturuki mpya. Erdogan alisema anatarajia kuifanyia mageuzi nafasi hiyo ya rais ili kumpa mamlaka zaidi, hatua ambayo inaweza kuipelekea Uturuki kuwa na mfumo kama wa Ufaransa, ikiwa chama chake cha haki na Maendeleo kitafanikiwa kuifanyia mabadiliko katiba.

Lakini wapinzani wa Erdogan wanamtuhumu kwa kudhoofisha mfumo wa mwanzilishi wa taifa hilo Mustafa Kemal Ataturk, ambaye alitenganisha dini na siasa alipoanzisha taifa hilo baada ya kuanguka kwa utawala wa Ottoman. Ihsanoglu, mkuu wa zamani wa jumuiya ya ushirikiano wa mataifa ya kiislamu OIC, alikubali kushindwa na kumpongeza Erdogan, lakini alisistiza kuwa kampeni yake ilikuwa na athari.

Wakati Waturuki wengi wasioegemea dini wanamchukia Erdogan, bado anaweza kutegeme uungwaji mkono kutoka sehemu kubwa ya wahafidhina wa dini wa tabaka la kati, hasa katikati mwa Uturuki, na wapigakura wa wilaya maskini za Istanbul, ambao wamepata mafanikio chini ya utawala wake.

Mgawanyo wa kura kikanda ulionyesha mgawiko wa wazi wa kijiografia nchini humo, huku Ihsanoglu akishinda katika pwani ya magharibi iliyo na wakaazi wengi wasioengemea dini, Demirtas akiungwa mkono zaidi na Wakurdi kuhini-mashariki, lakini Erdogan alishinda katika eneo la Bahari nyeusi, Istanbul na kanda yote ya katikati mwa taifa hilo.

Mgombea wa upinzani Ekmeleddin Ihsanoglu alikubali kushinda na kumpongeza Erdogan.
Mgombea wa upinzani Ekmeleddin Ihsanoglu alikubali kushinda na kumpongeza Erdogan.Picha: Reuters

Mabadiliko ya katiba

Erdogan alikuwa na kipindi kigumu zaidi cha utawala wake mwaka wa 2013, ukitikiswa na maandamano makubwa yaliosababishwa na mipango ya ujenzi wa maduka ya biashara katika bustani ya Gezi, ambayo yalipanuka na kuwa kilio cha jumla cha Waturuki wasioegemea dini waliohisi kutengwa na chama cha AKP.

Mustakabali wa rais anaemaliza muda wake Abdullah Gul, mwanzilishi mwenza wa chama cha AKP aliejitenga na Erdogan, hauko bayana. Waziri wa mambo ya kigeni Ahmet Davutoglu, anatazamiwa kuteuliwa kuwa waziri mkuu. Lakini wachambuzi wanaonya kuwa Erdogan anaweza kukabiliwa na wakati mgumu kubadilisha katiba ili kutoa mamlaka zaidi kwa rais.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe, rtre, dpae.
Mhariri: Daniel Gakuba