1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yataka kuumaliza mgogoro najirani yake Eritrea

Josephat Charo
8 Juni 2018

Wiki hii wahariri wamezungumzia matumaini yaliyochomoza katika eneo la pembe ya Afrika ambako waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameanzisha mchakato kabambe wa kuumaliza uhasama kati ya nchi yake na Eritrea.

https://p.dw.com/p/2zAJN
Äthiopien Addis Abeba Premierminister Abiy Ahmed
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy AhmedPicha: Reuters/T. Negeri

Gazeti la Neue Zürcher lilikuwa na kichwa cha habari kilichosema "Upepo mpya wavuma mjini Addis Ababa" - mkuu wa serikali ya Ethiopia ashangaza kwa hatua zake za mageuzi, hata wakosoaji wake.

Mhariri wa gazeti hilo alisema Ethiopia inataka kuufikisha mwisho mgogoro wa mpakani na jirani yake Eritrea. Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amekuwa madarakani kwa kiasi miezi miwili lakini tayari anaibadili nchi hiyo. Serikali yake imetangaza inataka kuufikisha mwisho mzozo wa mpaka na jirani wake mdogo na inakubali mkataba wa Algeria wa mwaka 2000 na makubaliano ya kimataifa ya mpaka ya mwaka 2002 bila masharti. Serikali ya Eritrea imetakiwa ichukue hatua kama hizo ili kurejesha tena amani.

Nalo gazeti la Süddeutsche Zeitung liliandika: Kwa miaka mingi Waethiopia na Waeritrea wamekuwa wakipigana. Sasa waziri mkuu wa Ethiopia amenyosha mkono wa amani kwa taifa jirani la Eritrea, lakini mhariri anasema swali linaloulizwa ni kama pendekezo lake litapokelewa.

Kuhusu Ethiopia gazeti la Süddetsche Zeitung liliandika kichwa cha habari kilichosema "Msimu wa machipuko Ethiopia".

Gazeti lilisema bunge la nchi hiyo siku ya Jumanne lilipiga kura na kupitisha kwa idadi kubwa ya kura kumaliza kipindi cha utawala wa hali ya hatari, na kuruhusu hali ya kawaida kurejea nchini. Mhariri wa gazeti la Süddeutsche anasema hata hivyo nchi hiyo inaendelea kubakia katika hali ya tahadhari, kati ya matumaini na wasiwasi, ambayo imewazonga Waethiopia wengi kati ya wakazi milioni 100 wa nchi hiyo. Hisia hazikuwa za kawaida katika Ethiopia ya miaka ya nyuma.

Ukuaji uchumi Afrika wasuasua

Uchumi Afrika haukui kwa kasi na nguvu inayotakiwa- Ndivyo lilivyoandika gazeti la Die Welt. Mhariri wa gazeti hilo alisema kunakosekana nafasi za ajira na idadi kubwa ya waafrika wanakimbilia Ulaya kutafuta maisha ya neema.

Libyen Flüchtlinge
Baadhi ya wahamiaji 104 waliookolewa na walinzi wa pwani ya Libya wakiwa njiani kuelekea UlayaPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la Die Welt lilisema mamilioni wameyakimbia makazi yao katika muongo mmoja uliopita, kutokana na hali ngumu ya kiuchumi kwenda kujitafutia kipato kwingineko. Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara UNCTAD hali haitarajiwi kubadilika. Ukuaji uchumi ni wa mwendo wa kinyonga.  Katika baadhi ya nchi za Afrika uchumi unakua kwa kasi nzuri, lakini sio kwa nguvu vile kiasi cha kuweza kuwanyanyua kiuchumi wananchi.

Katika eneo la kaskazini mwa Afrika ambako watu wengi hukimbilia Ulaya, theluthi moja ya vijana hawana ajira kwa mujibu wa takwimu za shirika la kimataifa la ajira, ILO. Katika eneo la Afrika Mashariki ambako Umoja wa Mataifa unatoa fedha kusaidia shuhguli za kiuchumi nchini Ethiopia, Kenya na Rwanda, ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana umepungua japo kidogo mwaka uliopita. Kwa ujumla ukosefu wa ajira katika maeneo yote ya Afrika mwaka uliopita umebaki pale pale.

Mapambano dhidi ya rushwa Afrika

Gazeti la Die Welt pia lilizungumzia "Terminator" na aina mpya ya viongozi wanaobeba matumaini barani Afrika. Mhariri alisema kusini mwa Afrika kuna upepo wa mageuzi unaovuma. Viongozi wapya wa serikali wanaonesha ukakamavu na wanakabiliana na ufisadi bila kutetereka. Vuguvugu jipya limeanza.

Mhariri wa gazeti la Die Welt anasema rais wa Angola Joao Lourenco alilishanga taifa lake katika miezi minane ya kwanza madarakani na shughuli nyingi za kila siku. Alituma picha katika mitandao ya kijamii, kwa mfano akitembea ufuoni bila walinzi, na akiwa katika mgahawa wa chakula. Hata gari lake liliposimama kwenye taa nyekundu barabarani, maelfu ya watu walitoa maoni yao, kwamba rais pia anaheshimu sheria zile zile wanazotakiwa kuziheshimu raia. Ni matumaini mapya katika taifa ambalo lilikuwa limedhibitiwa na rais wa zamani Jose Eduardo dos Santos.

John Magufuli Präsident Tansania
Rais wa Tanzania, John Pombe MagufuliPicha: picture-alliance/AA/B. E. Gurun

Lakini sio Lorenco tu. Nchini Tanzania rais John Magufuli amesimama kidete kupambana na rushwa, ingawa mhariri anasema ananyoshewa kidole cha lawama kwa kuukandamiza upinzani na mashirika ya kijamii. Pia nchini Afrika Kusini rais Cyril Ramaphosa amejitokeza kuupiga vita ufisadi licha ya changamoto zinazomkabili. Nchini Zimbabwe nako mwisho wa enzi ya rais wa zamani Robert Mugabe umeleta matumaini. Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amechukua mkondo wa mageuzi,akiupiga vita ufisadi na kujiepusha na kauli za chuki dhidi ya raia wa kigeni.

Gazeti la Neues Deutschland liliripoti kuhusu ufadhili wa Rwanda wa jezi za timu ya kandanda ya Arsenal London likisema ni sera muafaka ya kiuchumi inayostahili.

Mhariri wa gazeti hilo la Neues Deutschland anasema baadhi wanasema ufadhii huo wa timu ya Arsenal ya jijini London, Uingereza, unaolenga kuimarisha utalii ni kashfa ya kisiasa lakini Rwanda yenyewe inasema haijafanya kosa na ina haki ya kuwekeza mahala inapoona raia watapata manufaa. Mhariri aidha anasema ni suala lililo wazi ikiwa uwekezaji huo utasaidia Rwanda kuyafikia malengo yake ya kuwavutia watalii kuitembelea nchi hiyo chini ya kauli mbiu "Visit Rwanda" yaani Tembelea Rwanda.

Wafanyakazi wa KPMG watimuliwa

Kampuni ya uhasibu ya KPMG imewafuta kazi wafanyakazi wake 400 nchini Afrika Kusini. Hiyo ni taarifa iliyoripotiwa na gazeti la Frankfurter Allgemeine.

Mhariri wa gazeti hilo alisema kashfa ya rushwa katika kampuni hiyo ya "Klynveld Peat Marwick Goerdeler, KPMG, yenye makao yake makuu mjini  Amstelveen nchini Uholanzi, imesababisha athari kwa wafanyakazi. Kampuni hiyo itaendelea na shughuli katika afisi zake nne - mjini Johannesburg, Cape Town, Durban na Port Elizabeth. Afisi zote katika maeneo ya mikoani zitafungwa. Mkuu wa kampuni ya KPMG Afrika Kusini, Nhlamulo Dlomu, alizungumzia uamuzi mgumu ambao ulikuwa muhimu ili kuiimarisha tena kampuni hiyo.

Mwandishi: Josephat Charo/Pressedatenbanken

Mhariri: Daniel Gakuba