1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia lawamani kwa kukandamiza haki za binadamu

Kalyango Siraj13 Oktoba 2008

Shirika la Human Rights watch lataka ikabwe

https://p.dw.com/p/FYaU
Nembo ya shirika linalotetea haki za Binadamu

Serikali ya Ethiopia imelaumiwa na mashirika yananyotetea haki kwa kwenda kinyume na haki za binadamu kupitia sheria inayopanga kuhusu mashirika yasio ya kiserikali nchini humo.Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameomba bunge la nchi hiyo kuitupilia mbali sheria hiyo.

Lawama dhidi ya serikali ya Addis Ababa zimetolewa na shirika linalotetea haki za binadamu la Human Rights Watch katika taarifa yake lililoitoa jumatatu mjini New York nchini Marekani.

Lawama hizo zinafuatia hatua ya serikali ya Ethiopia kupanga kuwasilisha bungeni muswada mpya kuhusu mashirika yasiyoya kiserikali, katika lugha ya kigeni unaitwa The Charities and Societies Proclamation CSO Law.

Sheria ya CSO Law,kwa mujibu wa taarifa ya shirika la Human Rights Watch, itayapiga marufuku mashirika hayo yawe ya ndani mwa nchi hiyo au nje, yanayofadhiliwa kutoka nje kwa kiwango cha asili mia zaidi ya 10, kutoshughulika na masuala ya haki za binadamu, watoto, walemavu, masuala ya usawa wa kijinsia,kutanzua migogoro, na pia kuimarisha sheria na utekelezaji pamoja na shughuli zinazohusikana na masuala hayo.

Shirika la kutetea haki linaendelea kuwa sheria hiyo haitayaruhusu makundi ambayo, kwa kiwango kikubwa, yakifadhiliwa na raia wa nchi hiyo waishio ng'ambo,kujihusisha katika masuala yaliyotajwa hapo awali.

Human Rights Watch linasema kuwa sheria hiyo inapendekeza adhabu kali kwa wale watakaoikiuka ,mkiwemo kifungo cha miaka kati ya mitatu na mitano kwa kwenda kinyume na makosa madogomadogo ya kiutawala.

Shirika hilo linadai kuwa serikali ya Ethiopia inasema kuwa sheria, ambayo muswada wake ulifanyiwa marekebisho mara mbili tangu Mei 2008 lakini kubakisha sehemu nyingi zinazoshangaza,itachochea uwajibikaji.

Lakini mkurugenzi wa kitengo cha Afrika cha shirika la Human Rights Watch, Georgette Gagnon, katika taarifa iliotolewa na shirika hilo,ambayo miongoni mwa mengine inazitaka serikali hisani kulani ilichokiita shambulio dhidi ya haki, anasema kuwa, mataifa mengine ya kiafrika hufikia lengo hilo bila ya kupiga marufuku harakati za kupigania haki za binadamu.

Ameongeza kuwa sababu pekee ya sheria hiyo ni kuzikandamiza sauti pekee huru zilizosalia.Ameongeza kuwa serikali hisani ni lazima ziiambie wazi Ethiopia kuwa kupasisha sheria hiyo kutaathiri msaada wa hapo usoni.

Ameendelea kuwa Ethiopia, kama makao makuu ya Umoja wa Afrika ni lazima iwe msitari wa mbele katika juhudi za utawala bora badala ya kuongoza katika juhudi za ukandamizaji wa mashirika ya kijamii.

Taarifa ya shirika hilo imeendelea kudai kuwa sauti huru na zile zinazokosoa utawala wa Addis Ababa,kama vile upinzani wa kisiasa,tayari zinakandamizwa. Aidha linasema kuwa rikodi ya haki za binadamu ya nchi hiyo imeshapata doa na pia kuendelea kudidimia tangu uchaguzi mkuu wa 2005.Wakati huo vikosi vya usalama viliwauwa waandamanji wengi waliokuwa wanapinga matokeo ya uchaguzi huo.Na vilevile waandamanaji wengine maelfu kadhaa walikamatwa.

Hayo na mengine yamepelekea shirika hilo kutaka serikali hisani kuongeza mbinyo kwa serikali ili ikomeshe kuwaandama wanaharakati. Hata hivyo serikali hisani zimekataa kulaani hadharani ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Ethiopia,zikihoji kuwa mbinyo baridi ndio unafaa na unaozaa matunda.

Kila mwaka Ethiopia hupata msaada wa dola zaidi ya billioni moja.Taifa hilo linachukuliwa kama miongoni mwa yale maskini sana duniani.Isitoshe nchi hiyo ni mshirika mkuu katika vita vya Marekani na nchi za magharibi dhidi ya ugaidi wa kimataifa.