1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU, yaafiki kusaidia nchi zinazioendelea kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Halima Nyanza30 Oktoba 2009

Viongozi wa Umoja wa Ulaya leo wameafikiana juu ya kiasi gani cha fedha watatoa kwa nchi zinazoendelea kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa, lakini bila ya kusema kiwango cha fedha ambacho Ulaya itachangia.

https://p.dw.com/p/KJUP
Waziri Mkuu wa Swedish, ambaye nchi yake ndio Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya, Fredrik Reinfeldt (kulia) akiwa na Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso.Picha: DPA

Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya wamekubaliana kwamba nchi zinazoendelea zitahitaji kiasi cha Yuro bilioni 100, kuweza kukabiliana na kushughulikia matokeo ya mabadiliko ya hali ya hewa, hadi ifikapo mwaka 2020.

Hata hivyo viongozi hao wameshindwa kutaja kiwango cha fedha kitakachotolewa na bara la Ulaya, kutokana na tofauti kubwa ziliopo kati ya nchi masikini za Ulaya mashariki na mataifa tajiri ya magharibi.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Sweden, Fredrik Reinfeldt amesema Ulaya kwa sasa uko katika nafasi dhabiti ya kupatana kwa ajili ya kupata muafaka kuhusiana na suala la upunguzaji wa utoaji wa hewa chafu katika mkutano wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika Copenhagen, Denmark, Desemba mwaka huu.

Amesema nchi za Umoja wa Ulaya hazitahitaji kuchagia gharama hiyzo kabla ya mwaka 2013, zikiitikia matakwa ya nchi masikini za Umoja wa Ulaya.

Umoja wa Ulaya unataka kuanza kuonesha ari katika mazungumzo hayo ya Umoja wa Mataifa yatakayofanyika Copenhagen, kuhusiana na ujoto duniani kwa kuwa mataifa ya kwanza kuelezea jinsi yatakavyosaidia nchi masikini kupunguza utoaji wa gesi chafu.

Akisisitizia kuhusiana na mkutano huo wa Copenhagen, Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso alisema haya.

''...Kwa hakika, nafikiri kwa sasa tupo katika wakati muhimu sana. kuna watu wengi ambao wanaamini kwamba mkutano wa Copen hagen uko katika hatari.

Nafikiri, na tunafikiri, kwamba tunaweza kuufanya ukafanikiwa na Umoja wa Ulaya inafanya kazi yake ya uongozi kwa umakini mkubwa.....''

Fedha hizo ndio shina la kufanikisha mkutano huo wa Copenhagen, kutokana na kwamba nchi zinazoendelea zinasema kwamba hazitosaini makubaliano ya kukabiliana na uchafuzi wa hali ya hewa bila ya fedha za kutosha kutoka mataifa tajiri.

Katika hatua nyingine, viongozi wa nchi za Ulaya watajadili wagombea wa nafasi ya juu ya Urais katika kikao maalumu kitakachofanyika mwezi ujao.

Waziri Mkuu wa Luxembourg Jean-Claude Juncker amesema leo kwamba Waziri Mkuu wa Sweden Fredrik Reinfeldt amewaambia viongozi wenzake kwamba Sweden ambayo inashililia uenyekiti wa Umoja wa Ulaya itaanzisha mashaurino kuhusiana na uteuzi huo siku moja tu baada ya Rais wa Jamhuri wa Czech kusaini mkataba wa Lisbon.

Wakati huohuo, uwezekano wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair kuwa Rais wa kwanza wa Umoja wa Ulaya umefifia leo, baada ya kuonekana kutoungwa mkono na viongozi wengi wa umoja huo.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri:Abdul-Rahman