1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yaruhusu wasafiri kutoka mataifa 14 salama

Iddi Ssessanga
30 Juni 2020

Mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana juu ya kile yanachokiita "orodha salama" kwa mataifa 14 ambayo yataruhusiwa kwa safari zisizo muhimu kuanzia Julai, huku Marekani ikiwa haimo kwenye orodha hiyo.

https://p.dw.com/p/3eb1R
Symbolbild EU-Einreisebeschränkungen sollen für viele Länder bestehen bleiben
Picha: picture-alliance/NurPhoto/N. Economou

Baraza la Umoja wa Ulaya limesema hivi leo kwamba nchi hizo salama ni Algeria, Australia, Canada, Georgia, Japan, Montenegro, Morocco, New Zealand, Rwanda, Serbia, Korea Kusini, Thailand, Tunisia na Uruguay.

Kundi hilo la mataifa 27 linatazamiwa kutoa muongozo unaolegeza au kuruhusu safari za matembezi ama kibiashara kuanzia siku ya Jumatano kwa mataifa hayo. Urusi na Brazil, kama ilivyo Marekani, hazikukidhi vigezo vya mataifa yaliyo salama kutokana na janga la COVID-19.

Symbolbild EU-Einreisebeschränkungen sollen für viele Länder bestehen bleiben
Mataifa ya Ulaya yalioathirika zaidi na covid-19 yana shauku ya kuvutia tena watalii hasa msimu huu wa kiangazi.Picha: picture-alliance/NurPhoto/N. Economou

Uamuzi huu unakusudia kuunga mkono sekta ya usafiri na utalii barani Ulaya, hasa kwa mataifa ya kusini, ambayo yameathirika vibaya na janga la corona. Wakati mataifa ya Ulaya yakipambana na athari za virusi vya corona kwenye uchumi wake, mataifa kama Ugiriki na Uhispania yana shauku ya kuwavutia tena watalii kurudisha uhai katika chumi zao.

Watalii wa Kimarekani wanaunda sehemu kubwa zaidi ya soko la Umoja wa Ulaya na kipindi cha msimu wa kiangazi ni muhimu sana. Umoja wa Ulaya umesema China itaruhusiwa ikiwa tu na yenyewe itawaruhusu kwanza raia wa kanda hiyo kusafiri nchini humo.

Orodha hiyo inarekebishwa kila baada ya siku 14, ambapo mataifa mapya yatakuwa yanajumlishwa au kuondolewa kutegemea na iwapo yanaendelea kudhibiti mripuko wa ugonjwa wa covid-19.