1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FBI yachunguza mawasiliano kati ya Urusi na Trump

20 Machi 2017

Mkurugenzi wa Shirika la upelelezi nchini Marekani, FBI, James Comey, amethibitisha Jumatatu (20.03.2017) shirika hilo linachunguza uwezekano wa serikali ya Urusi kuuingilia uchaguzi wa Mareakani 2016

https://p.dw.com/p/2ZZTu
USA James Comey FBI Director Anhörung in Washington
Picha: Reuters/J. Roberts

Comey aliiambia kamati ya bunge inayohusika na masuala ya ujasusi leo kwamba uchunguzi wa shirika hilo utajumuisha mfumo wa mafungamano yoyote kati ya watu wanaohusihwa na timu ya kampeni ya rais Donald Trump na serikali ya Urusi na ikiwa kulikuwa na uratibu wowote kati ya timu hiyo na shughuli za Urusi.

Akizungumza mbele ya kamati hiyo, Comey alisema uchunguzi huo ni sehemu ya kazi ya kijasusi ya Shirika la FBI na atachunguza ikiwa uhalifu ulifanyika.

Mkurugenzi wa Shirika la usalama wa taifa NSA, Mike Rogers, pia anatoa taarifa mbele ya kamati hiyo ya bunge. Hii ni mara ya kwanza kwa wakuu hao wawili wa mashirika ya ujasusi kuzungumza hadharani kuhusu uchaguzi wao juu ya uwezekano wa mafungamano kati ya Urusi na timu ya kampeni ya rais Trump. Urusi inakanusha ilijaribu kushawishi matokoe ya uchaguzi wa Marekani Novemba mwaka uliopita.

Kwa upande mwingine Comey amekanusha madai ya Trump katika mtandao wa Twitter kwamba mtangulizi wake rais Barack Obama aliamuru mawasiliano yak ya simu yafuatiliwe katika jumba la Trump Tower kabla uchaguzi. Mkuu wa Shirika la NSA Mike Rogers pia amekanusha madai ya utawala wa Trump kwamba shirika hilo lililiomba Shirika la ujasusi la Uingereza kumchunguza rais huyo wa Marekani.

Mwandishi:Josephat Charo/reuters/afpe

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman