1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Federer ndiye Mfalme wa Wimbledon

Bruce Amani
17 Julai 2017

Katika Tennis, Mswisi Roger Federer aliweka rekodi kwa kushinda taji la Wimbledon na kuwa bingwa mwenye umri mkubwa zaidi wa dimba hilo hapo jana alipomwangusha Marin Cilic.

https://p.dw.com/p/2ggoB
Wimbledon 2017 | Finale Herren | Sieger Roger Federer
Picha: Getty Images/J. Finney

Federer alitwaa taji lake kuu la Grand Slam la 19 kwa seti za moja kwa moja za 6-3,6-1 na 6-4 na kwa kuwa ana umri wa miaka 35, ndiye bingwa wa Wimbledon mwenye umri mkubwa zaidi kwa upande wa wanaume katika enzi ya sasa. "Ndiyo, ni wa kipekee, Wimbledon kila mara huwa dimba nnalopenda sana, na litaendelea kuwa dimba bora kwangu. mashujaa wangu walitembea hapa na wakacheza hapa na kwa sababu yao nahisi nimekuwa mchezaji bora pia hivyo kuweka historia hapa Wimbledon nadhani ni muhimu sana kwangu".

Hata hivyo, fainali hiyo ya 11 ya Mswisi huyo, pia itakumbukwa na tukio la kutiririkwa machozi mpinzani wake katikati ya mchezo. Mcroatia Cilic, ambaye ni bingwa wa taji la US Open mwaka wa 2014, alititirikwa machozi wakati mambo yalionekana kumwendea mrama. Aliicheza fainali hiyo akiwa na maumivu kwenye mguu wake wa kushoto.

Katika upande wa wanawake, Garbine Muguruza mwenye umri wa miaka 23 alitwaa taji lake la kwanza la Wimbledon baada ya kumbwaga bingwa mara tano Venus Williams

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Yusuf Saumu