1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fiat yasusia kikao...Opel itasalimika?

29 Mei 2009

Wawakilishi wa Ujerumani na Marekani wako katika harakati za kuuokoa mpango wa kuikwamua kampuni ya magari ya Opel baada ya mazungumzo ya awali kuvunjika bila ya mwafaka wowote.

https://p.dw.com/p/Hzyp
Nembo ya FIATPicha: AP

Moja ya kampuni za wawekezaji, FIAT ya Italia, imetangaza kuwa inasusia kiakao cha leo kilichopangwa kuongozwa na Kansela Angela Merkel. Kampuni za FIAT na Magna ya Canada ndizo mbili pekee zinazoshindaha kuinunua kampuni ya Opel. Kwa upande mwengine, kampuni mama ya General Motors ya Marekani inajitahidi kutotangaza kuwa imefilisika.


Kampuni ya FIAT ya Italia imetangaza kuwa imejiondoa katika mazungumzo muhimu yaliyopangwa kufanyika mchana wa leo. Kwa mujibu wa taarifa iliyotokea Turin,wawakilishi wa FIAT kamwe hawatohudhuria kikao hicho cha Berlin kilichopangwa kuongozwa na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel. Mkutano huo ulikuwa na azma ya kuwaleta pamoja wawakilishi wa kampuni mama ya General Motors pamoja na wale wa wawekezaji wawili watarajiwa. Wawekezaji hao watarajiwa ni FIAT ya Italia na kampuni ya vipuri ya Magna iliyo na makao yake makuu Canada.




Spitzengespräch zu Opel im Kanzleramt
Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Karl-Theodor zu GuttenbergPicha: AP

Mazungumzo ya awali yalivunjika bila ya mwafaka wowote kufikiwa hapo jana baada ya kampuni mama ya General Motors kutoa tamko la kutaka fedha zaidi, jambo lililowashangaza wawakilishi wa Ujerumani. Kulingana na General Motors, fedha hizo zinahitajika ili kufadhili operesheni zake katika bara la Ulaya. Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Karl-Theordore zu Guttenberg, alisema kuwa walishangazwa na hatua hiyo.



Kulingana na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya magari ya Italia ya FIAT, Sergio Marchionne, dai hilo jipya la General Motors huenda likaifanya kampuni yake kufadhili shughuli za kampuni ya Opel, jambo ambalo litaiweka katika hali ya hatari ambayo inaweza kuepukika. Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Karl-Theodore zu Guttenberg, ameweka bayana kuwa kuna haja ya wawekezaji wote watarajiwa kuimarisha harakati zao za kutaka kuinunua kampuni ya Opel, vinginevyo italazimika kutangaza imefilisika.

Mazungumzo ya leo yatajikita katika juhudi za kufidia kiwango kipya cha Euro milioni 300 kilichowasilishwa na kampuni ya General Motors siku ya Jumatano. Serikali ya Ujerumani inapanga kuzikomboa operesheni za kampuni ya Opel kwa kuipa mkopo wa Euro bilioni 1.5 utakaosimamiwa na bodi ya muda ya wadhamini.


Symbolbild Opel GM
Nembo ya OpelPicha: AP&DW

Kwa upande mwengine baraza la wafanyakazi la Opel limevunjwa moyo baada ya mazungumzo hayo kuvunjika bila ya mwafaka wowote kufikiwa.Viongozi wa baraza hilo wameilaumu kampuni ya General Motors kwa kuipa kampuni ya Opel uzito mdogo ukizingatia hali halisi.

Marekani, kwa upande wake, imekanusha madai hayo.

Katika hatua ambayo haikutarajiwa kampuni ya General Motors iliihamishia Opel mali zake zote pamoja na hataza-kibali maalum cha kutengeza bidhaa zake- kwa minajili ya kuzilinda endapo kampuni mama itafilisika.

Kutokana na hilo, mpango mpya wa kuiokoa kampuni ya General Motors ulizinduliwa na kuiwezesha serikali ya Marekani kuwa na asilimia 72.5 ya hisa zote. Rais Obama amesisitiza kuwa hatua hiyo ina azma ya kuiokoa kampuni hiyo tu.


Kampuni ya General Motors, kwa upande wake. imeahidi kuzihamishia Opel mali za kiwanda cha Vauxhall na vitengo vyengine vyake vilivyoko barani Ulaya mpaka pale mwekezaji atakapopatikana.

Wawekezaji nao wanataraji kuwa serikali ya Ujerumani itafadhili kiasi cha zaidi ya euro bilioni 5 kama malipo ya uzeeni na fidia kwa wafanyakazi.

Kamisheni ya Umoja wa Ulaya imeionya serikali ya Ujerumani kuzingatia sheria za Umoja huo inapoendelea na harakati za kuikwamua kampuni ya Opel.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya

Mhariri:Othman Miraji