1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FIFA yamsimamisha katibu mkuu wake

Admin.WagnerD18 Septemba 2015

Shirikisho la kandanda ulimwenguni FIFA limemsimamisha kazi katibu mkuu wake Jerome Valcke kwa madai ya kujihusisha na masuala ya rushwa ndani ya shirikisho hilo.

https://p.dw.com/p/1GYXz
Katibu mkuu wa FIFA, Jerome Valcke.
Katibu mkuu wa FIFA, Jerome ValckePicha: picture-alliance/epa/A. Della Bella

Valke ambaye ni mshirika mkuu wa Rais wa shirikisho hilo ambaye muda wake wa uongozi unamalizika Sepp Blatter alivuliwa mara moja nyadhifa zake ndani ya shirikisho hilo mara tu baada ya kufichuliwa kwa kashifa hiyo.

Kiongozi huyo ambaye ni raia wa ufaransa mwenye umri wa miaka 54 alisimamishwa hapo jana kufuatia taarifa zilizoandikwa katika magazeti zikimuhusisha na sakata la kuuza kwa njia ya ulanguzi maelfu ya tiketi zilizotumika wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka jana madai ambayo ameyakanusha. Mlolongo wa shutuma za aina hiyo ndio uliopelekea pia hatua ya Rais wa FIFA Sepp Blatter kuchukua uamuzi wa kujiuzulu wadhifa huo siku chache tu baada ya kuchaguliwa kwake kwa muhula mwingine wa tano wa uongozi ndani ya shirikisho hilo.

Ahusishwa pia na kashifa ya kuipendelea Afrika ya kusini

Valke pia anahusishwa na sakata la kiasi cha fedha chenye thamani ya dola milioni kumi sawa na fedha zenye thamani ya sarafu ya euro milioni 9.1 ambayo ni malipo yaliyofanywa na shirikisho la kandanda la afrika ya kusini katika akaunti ya fedha inayodhibitiwa na kiongozi mkuu wa shirikisho la kandanda la ukanda wa Amerika ya kati na kaskazini (CONCACAF) Jack Walner kupitia FIFA mnamo mwaka 2008.

Wachunguzi wa suala hilo wanadai fedha hizo zilikuwa ni rushwa kama shukrani ya kuiunga mkono Afrika ya kusini katika kupata nafasi ya kuandaa fainali za kombe la dunia za mwaka 2010.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusiana na kashifa hiyo alisema.

Valke ambaye pia ana uraia wa Afrika ya kusini kama mkewe amedai kuwa alikuwa na taarifa tu kuhusiana na malipo hayo kwa vile mawasiliano yote yanayohusiana na FIFA yalipitia kwake kama katibu mkuu lakini akakanusha kuidhinisha malipo hayo.

Hatua ya kusimamishwa kwa katibu mkuu huyo ambaye pia ni mwandishi wa habari kitaaluma inaelekea kufifisha nyota yake ya kungara kimadaraka ndani ya shirikisho hilo.

Alianza majukumu yake ya uandishi wa habari katika kituo cha televisheni cha Ufaransa 1984 na baadaye kushika nyadhifa mbalimbali za juu katika vyama vya michezo kabla ya kuteuliwa kuwa mkurugenzi wa masoko wa FIFA mwaka 2003 na baadaye tena kuteuliwa kuwa katibu mkuu wa shirikisho hilo.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE

Mhariri :Yusuf Saumu