1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Frankfurt washerehekea kombe la DFB Pokal

Bruce Amani
21 Mei 2018

Eintracht Frankfurt ilisherehekea pamoja na mashabiki wake mjini Frankfurt baada ya kuwaacha hoi Bayern Munich kwa kuwacharaza 3-1 katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Ujerumani – DFB Pokal

https://p.dw.com/p/2y4Gi
Fußball Eintracht Frankfurt gewinnt DFB-Pokal
Picha: picture-alliance/dpa/A. Dedert

Ulikuwa ushindi wao wa tano wa kombe hilo na hivyo kuwanyima wapinzani wao fursa ya kushinda mataji mawili ya nyumbani msimu huu wakati kocha wao Jupp Heynckes akistaafu.

Mwalimu wa Frankfurt Niko Kovac, ambaye atachukua usukani wa Bayern msimu ujao, alilinyanyua juu kabisa kombe hilo la kwanza kwa Frankfurt katika miaka 30, wakati mashabiki wakifyatua fataki na mabomu ya moshi kwa furaha. Kiungo wa Frankfurt Alexander Meier alielezea furaha yake "sijui niseme nini, kwa mazingira haya - nimekuwa hapa kwa muda mrefu lakini sijawahi kushuhudia kitu kama hiki. tunajivunia sana mashabiki wetu. vijana walipambana sana uwanjani jana na nadhani tulishinda kwa haki baada ya miaka 30. sijui niseme nini. ahsanteni! ahsanteni!"

Fußball Eintracht Frankfurt gewinnt DFB-Pokal
Mashabiki wa Frankfurt wakiwashangilia wachezajiPicha: picture-alliance/dpa/F. Rumpenhorst

Na wakati hayo yakiendelea mjini Frankfurt, jimboni Bvaria mjini Munich maelfu ya mashabiki wa Bayern walijitokeza kumuaga Jupp Heynckes kwa mara ya pili.

Kocha huyo mkongwe anastaafu baada ya kuiongiza Bayern kutwaa taji jingine la ligi kuu – Bundesliga. Heynckes mwenye umri wa miaka 73 aliwapongeza mashabiki kwa kujitokeza licha ya matokeo ya fainali ya DFB Pokal "sasa kuna pongezi za kutosha, hatuzungumzi tena kuhusu mimi, bali kuhusu nyie mashabiki na timu yangu. Kwa sababu nadhani nyie, kama tu tulivyo sisi, mmesikitishwa na mchezo wa jana, kichapo. Lazima niseme sikutarajia kuona kinachoendelea hapa leo. kuna mashabiki wengi hapa wanaosherehekea, inapendeza sana.

Fußball Bundesliga FC Bayern München Jupp Heynckes
Jupp anastaafu kwa mara ya pili Picha: picture-alliance/dpa/T. Hase

Mshambuliaji wa Bayern Thomas Müller alisema inasikitisha sana jinsi msimu ulivyokamilika kwa kichapo "bila shaka tulikuwa na mawazo na hisia tofauti wiki tatu, nne zilizopita, kuwa tungeweza kushinda kitu kikubwa. tulicheza kwa kujiamini sana mwezi mzima wa Apili na sasa tupo hapa tukiwa na taji la ligi pekee, tulipoteza Kombe la Ujerumani jana, na kisha tukajiambia kama timu, ooh itakuwa vigumu sana tutakapoenda Munich, lakini unapoona watu waliojitokeza hapa basi tunafurahi tu kwa uungaji mkono wenu.

Heynckes aliiongoza Bayern kutwaa Kombe la Mabingwa Ulaya na mataji mawili ya Ujerumani – Bundesliga na DFB katika uongozi wake wa awali mwaka wa 2013 kabla ya kustaafu kwa mara ya kwanza.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP
Mhariri: Mohamed Khelef