1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FRANKFURT:Waziri wa mipango wa Rwanda wa zamani akamatwa

20 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBOL

Waziri mmoja wa zamani wa Rwanda anayesakwa kwa kuhusika na mauaji ya halaiki ya mwaka ‘94 amekamatwa hapa Ujerumani.Waziri huyo wa mipango wa zamani anashukiwa kuchagiza mauaji ya WaTutsi walio wachache kwa kuwapa silaha wapiganaji wa KiHutu kwa mujibu wa msemaji wa polisi.

Kulingana na msemaji huyo mshukiwa huyo aliye na umri wa miaka 50 alikamatwa karibu na mji wa Frankfurt ikiwa ni ombi la Mahakama ya kimataifa kwa ajili ya Rwanda ICTR.Msemaji wa mahakama hiyo Roland Amoussouga anathibitsha kuwa aliyekamatwa ni waziri wa zamani ajulikanaye kama Augustin Ngirabatware.Jina la waziri huyo wa zamani lipo katika orodha ya washukiwa wanaosakwa wa mauaji ya mwaka 94.

Waziri wa Sheria wa Rwanda Tharcisse Karugarama anapongeza hatua hiyo na nchi yake inapanga kudai haki kwa mshukiwa huyo kurejeshwa nchini mwake ili kujibu mashtaka.Polisi wa hapa Ujerumani walianzisha msako huo mwezi Julai.Hata hivyo mahakama ya Ujerumani ilielezea shirika la habari la AFP kuwa hatua ya kumrejesha mshukiwa huyo huenda ikachukua muda mrefu kwani huenda akawasilisha kesi rasmi kuipinga.

Bwana Ngirabatware alikuwa waziri wa mipango kwa miaka mine kabla mauaji ya halaiki kutokea mwaka 94 na kuishi nchini Gabon na Ufaransa kwa muda mrefu.Itakumbukwa kuwa mshukiwa huyo ni mkwe wake Felicien Kabuga mfanyabiashara mkubwa na mshukiwa anayesakwa na mahakama ya kimataifa ya ICTR.Inaaminika kuwa Bwana Kabuga ndiye aliyefadhili vyombo vya habari vilivyochagiza mauaji hayo ya halaiki.watu takriban laki 8 walipoteza maisha yao katika mauaji hayo ya siku 100.Mahakama hiyo ya ICTR iliyoko mjini Arusha nchini Tanzania imewapata na hatia washukiwa wakuu 28 na kuwaachia 5 tangu ilipoanzishwa.