1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G8: Misaada ya maendeleo iongezwe

Kujath, Peter7 Aprili 2008

Licha ya kuwa utoaji wa misaada ya maendeleo kuwa umeshuka chini duniani kote, nchi saba zinazoongoza kiviwanda duniani na Urusi, yaani kundi linalojulikana kama G8, bado zinataka kutekeleza ahadi zao kuelekea Afrika.

https://p.dw.com/p/Ddji
Malengo ya millenia yanataka umaskini upunguzwe kwa nusu hadi mwaka 2015Picha: AP

Haya yaliarifiwa na mawaziri wa mambo ya maendeleo wa nchi hizo nane kwenye mkutano waliofanya jijini Tokyo, Japan, kama alivyoeleza waziri wa masuala ya maendeleo wa Ujerumani, Bi Heidemarie Wieczorek-Zeul: “Mawaziri wa maendeleo wa nchi za G8 waliweka wazi kwamba ahadi walizozitoa kwa nchi za Kiafrika watazitekeleza. Hii ni hatua muhimu tukiangalia takwimu ambazo zinaonyesha misaada ya maendeleo haikuongezwa.”


Ni sauti ya Bibi Heidemarie Wieczorek-Zeul, waziri wa masuala ya maendeleo na ushirikiano wa kiuchumi wa Ujerumani akiongea kwenye mkutano na mawaziri wenzake wa nchi za kundi la G8. Changamoto kubwa, mawaziri hao walikabiliwa nayo ni upunfugu katika malipo ya misaada ya maendeleo katika dunia kwa ujumla. Kulingana na takwimu, bajeti ya maendeleo ilipunguzwa hadi kufikia Dola Billioni 103,6. Tukilinganisha takwimu hizo na matumizi kwa ajili ya jeshi, idadi ni mara kumi kubwa kuliko matumizi kwa misaada ya maendeleo. Ndiyo sababu, waziri wa masuala ya kigeni wa Japan alisema, serikali yake ambayo kwa miaka hii ni mwenyekiti wa kundi la G8 inalenga kuhakikisha misaada ya maendeleo inaongezwa.


Ujerumani inatoa asimilia 0.37 ya pato la taifa kama misaada ya maendeleo na hivyo imetekeleza ahadi zake. Nchini Japan lakini mchango huo umepungua hadi asilimia 0.17, na huko Marekani ni asilimia 0.16 ya pato la taifa inayotumika kama misaada ya maendeleo. Hata hivyo, mawaziri waliokutana Tokyo wanataka malengo ya Millenia yaliyokubaliwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa yatimizwe.


Waziri Wieczorek-Zeul wa Ujerumani alisisitiza kuwa malengo haya ni suala la uaminifu, lakini kama mawaziri hawana njia nyingine ila kukumbusha juu ya malengo haya na kulaumu rasmi ikiwa malengo hayatafikiwa. Miongoni mwa malengo manane ya Millenio yaliyokubaliwa hapo mwaka wa 2000 ni kupunguza kwa nusu idadi ya watu maskini, kupiga vita magonjwa kama Ukimwi, Malaria na kifua Kikuu, na kupunguza idadi ya akinamama na watoto wanaokufa wakati wa uja uzito na baada ya kuzaa au kuzaliwa. Juu ya hayo, nchi za G8 hapo mwaka wa 2005 zimeamua kuongeza kwa mara mbili misaada ya maendeleo.


Huyu hapa tena waziri Heidemarie Wieczorek-Zeul: “Lengo kuu ni kupunguza umaskini mkali duniani. Na likiwa ni suala muhimu kuhusiana na hilo tulizungumzia pia ongezeko la bei za vyakula. Mimi binafsi ninatoa kipaumbele kupambana na kashfa hiyo ya kwamba idadi ya watoto wanaokufa wakiwa bado wadogo ni kubwa. Kila siku, watoto 26.000 ambao hawajafika umri wa miaka mitano wanakufa.”


Pamoja na nchi nane zilizostawi kiviwanda, walioalikwa pia kwenye mkutano huo wa Japan ni wajumbe wa nchi zinazokuwa haraka kiuchumi, yaani China, India na Brazil. Hususan Chini ililaumiwa kwa kufuatia maslahi yake ya kibiashara tu na kutojali haki za binadamu katika kugawa misaada yake ya maendeleo.