1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G8 ni jinamizi au faida kwa dunia?

Sandra Petersmann / Maja Dreyer23 Januari 2007

Kwenye kongamano la kimataifa kuhusu masuala ya kijamii linaloendelea mjini Nairobi, Kenya, kuna neno moja linalorudiwa mara kwa mara, ikiwa ni katika mazungumzo juu ya tatizo la maji, haki za wanawake au mizozo. Neno hili ni G8, yaani jina fupi la kundi la nchi nane zinazoongoza kiviwanda duniani. Wengi wa wanaohudhuria wanaona kundi hili ndio msingi wa maovu ya utandawazi, wengine lakini wanataka kushirikiana na nchi za G8.

https://p.dw.com/p/CHlk
Maandamamo kwenye kongamano la Nairobi
Maandamamo kwenye kongamano la NairobiPicha: AP

“Ikiwa mimi ningekuwa mwanachama wa G8, basi ningejiuliza kwa njia gani naweza kuihudumia dunia hii, na siyo kuuliza duniani hii itaninufaisha vipi. Ikiwa una mamlaka mkubwa, ni juu yako kuamua juu ya maisha ya watu wengine. Lakini kuwepo mafaa haya mengi, kunazipa sifa mbaya nchi za G8.”

Anayesema haya ni Bibi Rathindra Roy, mwanaharakati dhidi ya utandawazi kutoka India. Mjumbe mwingine kutoka India ana maoni makali zaidi. Ni Vandana Shiva, mwandishi na mwanaharakati wa mazingira ambaye alipata umaarufu mkubwa tangu kongamano la kwanza la kimataifa kuhusu masuala ya kimataifa kufanyika nchini Brasil mnamo mwaka 2001. Kwa maoni yake, G8 ni kundi lisilo la kidemokrasi, halina murua, na ni hatari kwa dunia.

Amesema:“Tuangalie nyuma kidogo na tuizingatie miaka 15 ya biashara huru duniani, miaka 10 ya shirika la biashara duniani na miradi ya kubadilisha mifumo ya kiuchumi kwa nchi maskini ya benki ya dunia. Hebu mnaona, vile mizozo ilivyozidi? Mnaona, vile ugaidi umezidi na utoaji wa gesi chafu kuongezeka na kuibadilisha hali ya hewa? Hatutaki jinamizi hili la G8 lipewe chakula zaidi ili liweze kuharibu maisha mengi zaidi.”

Badala ya kutegemea mashirika makubwa ya kifedha au nchi tajiri kama G8, Vandana Shiva anasisitiza nguvu ya jamii ya kimataifa na kutaka usawa katika ugawaji wa rasili mali pamoja na mfumo wa kidemokrasi unaowashirikisha watu wote.

Maoni tofauti anayo Immanuel Lowilla kutoka Sudan ya Kusini. Mwanaharakati huyu wa haki za binadamu aliyewahi kuona vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe analitambua kundi la G8 akisema: “Hili ni kundi la nchi tajiri ambazo zilijitolea kushirikiana kwa ajili ya kuowanisha hatua zao. Naamini zinaweza kuboresha hali ya dunia hii, kwa vile zinazo kile zinachohitaji. Hatuna haki ya kudai kundi hili lisitishwe, lakini yale tunataka kusema ni kwamba nchi hizi zitumie mamlaka yao kuinufaisha dunia nzima.”

Dai lingine linalosikika kwenye kongomano la Nairobi ni kutaka siasa wazi katika kundi la G8. Ikiwa viongozi hawa wanashindwa kuweka wazi siasa zao na kuipiga vita rushwa katika nchi zao, basi raia wa mataifa ya Kiafrika pia watashindwa kuzidhibiti serikali zao.