1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gabon yaomboleza

9 Juni 2009

Nchi ya Gabon inaomboleza baada ya rais wan chi hiyo marehemu Omar Bongo Ondimba kufariki hapo jana katika hospitali moja ya binafsi nchini Uhispania.Maiti yake inatarajiwa kusafirishwa hadi Gabon ifikapo Ijumaa.

https://p.dw.com/p/I66T
Marehemu Rais wa Gabon Omar BongoPicha: picture-alliance/dpa


Wakati huohuo Waziri wa Ulinzi wa Gabon Ali Ben Bongo aliye pia mwanawe marehemu ametoa wito wa kudumishwa amani katika kipindi hicho kigumu.Baadhi ya viongozi wa kimataifa wametoa rambirambi zao vile wamempongeza marehemu rais Bongo aliyeshika wadhifa huo kwa muda mrefu zaidi barani Afrika.


Kifo hicho kilitangazwa rasmi na Waziri Mkuu wa Gabon Jean Eyeghe Ndong hapo jana jioni.Punde baada ya hapo serikali ilitangaza kuanza kwa kipindi cha siku 30 za maombolezi ya kitaifa ambapo bendera zote zitapeperushwa nusu mlingoti.Maiti ya marehemu rais imepangwa kusafirishwa hadi Libreville hapo Ijumaa.Maziko rasmi yanatarajiwa kufanyika kati ya Ijumaa hiyohiyo na tarehe 15 mwezi huu wa Juni.Katika taarifa yake aliyoitoa kupitia kituo cha taifa cha televisheni Waziri wa Ulinzi wa Gabon Ali Ben Bongo aliye pia mwanawe marehemu ametoa wito wa amani kudumishwa katika kipindi hicho kigumu.Wizara ya Ulinzi kwa upande wake iliamua kuifunga mipaka yote ya nchi hiyo.

Marehemu rais Bongo alikuwa akipata matibabu ya saratani ya utumbo katika hospitali moja ya binafsi mjini Barcelona,Uhispania.Itakumbukwa kuwa kiongozi huyo mkongwe aliyeingia madarakani mwaka 1967 ndiye aliyeshika wadhifa huo kwa muda mrefu zaidi barani Afrika.

Viongozi wa bara la Afrika pamoja na wa kimataifa wametoa rambirambi zao.


Umoja wa Afrika wa upande wake umetoa rambirambi zake pamoja na Jamhuri ya Afrika ya Kati,Congo-Brazaville,Ivory Coast,Morocco,Senegal pamoja na waasi wa kundi la UFR lililoko Chad.Kamishna wa masuala ya amani na usalama wa Umoja wa Afrika Ramtane Lamamra alyiezungumza na shirika la habari la AFP alisema kuwa bara la Afrika limempoteza mtu muhimu.Kamishna huyo alisema kuwa ana imani kifo cha marehemu rais Bongo kamwe hakitochochea matatizo yoyote ya kikatiba wakati ambapo nchi inasubiri kupata kiongozi mpya.Hali inaripotiwa kuwa shwari nchini Gabon hata baada ya maduka na biashara muhimu kufungwa punde baada ya kifo hicho kutangazwa.Ifahamike kuwa Ali Ben Bongo mwanawe marehemu rais aliye pia waziri wa ulinzi anatarajiwa kuchukua nafasi hiyo. Faustin Boukoubi ni Katibu Mkuu wa chama tawala cha Demokrasia anaelezea kuwa''Chama cha Demokrasia cha Gabon kimesikitishwa sana na kifo cha ndugu yetu Omar Bongo ambaye filosofia yake ilikuwa ni amani.Sisi tunaheshimu sheria na katiba itadumishwa kwa hali zote.'' anamaliza.

Rais wa Marekani Barack Obama aliyetuma rambirambi zake alisema kuwa marehemu rais alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha uhusiano uliopo kati ya nchi zao mbili.Rais Obama alisisitiza kuwa marehemu alikuwa kiongozi aliyechangia katika harakati za kutatua mizozo kote barani Afrika.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon naye pia alimsifu marehemu na kuafiki matamshi hayo.Rais wa Venezuela Hugo Chavez naye pia alituma rambirambi zake kwa familia ya marehemu .


Rais Bongo aliingia madarakani mwaka 1967 na aliungwa mkono na Ufaransa.Itakumbukwa kuwa katika miezi ya mwisho kabla ya kufariki kwake marehemu rais alizozana na Ufaransa baada ya madai ya rushwa na ufisadi kumzonga.Kwa mujibu wa wanaharakati marehemu alihusika na vitendo vya ubadhirifu ndipo akaweza kuyanunua majengo ya kifahari Ufaransa.


Mwezi Februari mwaka huu mahakama ya Ufaransa iliamua kuzuwia fedha zilizokuwa kwenye akaunti zake za benki jambo lililoighadhabisha serikali ya Gabon iliyodai kuwa ni njama ya kuiyumbisha nchi.Hata hivyo kulingana na mwanasheria wa Ufaransa kifo cha marehemu rais Bongo hakitabadili chochote ukizingatia misingi ya kisheria kwani familia yake ndiyo itakayowajibika katika kesi hiyo ya rushwa.Gabon ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa mwenyeji wa kampuni ya mafuta ya Ufaransa ya Elf katika miaka ya 1960.Katika kipindi hicho Ufaransa iliendesha shughuli zake bila yakuingiliwa na serikali hususan katika masuala ya kijeshi na ujasusi.


Mwandishi:Thelma Mwadzaya AFPE/RTRE

Mhariri: M.Abdul-Rahman