1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaddafi aapa kupambana mpaka mwisho

Admin.WagnerD23 Machi 2011

Ikiwa imetimia siku nne ya mashambulizi ya nchi za magharibi nchini Libya, kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi, amesema mabavu yao hayatafanikiwa katika vita hivyo na kwamba atapambana mpaka hatua ya mwisho.

https://p.dw.com/p/10gAC
Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi
Kiongozi wa Libya Muammar GaddafiPicha: AP

Gaddafi alitoa kauli hiyo, huku vikosi vyake vikiendelea na mashambulizi katika maeneo ya waasi bila ya kuhofia makombora ya Marekani, Ufaransa na Uingereza ambayo leo yamevurumishwa katika maeneo kadhaa ya Tripoli.

Waliyoshuhudia wanasema, miripuko ya makombora kutoka katika ndege za kivita imesikika.

Katika mashambulizi hayo,inadaiwa majeshi ya nchi za Muungano yamefanikiwa kuiangusha ndege moja ya Gaddafi na kuyarudisha nyuma majeshi yake kutoka ngome ya upinzani huko Benghazi.

Ndege ya kijeshi ya Marekani
Ndege ya kijeshi ya MarekaniPicha: US Air Force/TSgt. John K. McDowell

Tathimini inaonesha kwa, vikosi vya waasi vinashindwa kumudu kishindo cha Gaddafi kutokana na kuwa na mpangilio duni wa kivita pamoja na kutokuwa na vifaa vya kisasa.

Gaddafi mwenyewe amesikika akiwaambia watu wanaomuunga mkono mjini Tripol,"tutawashinda kwa nanma yeyote", kwamba wao wapo tayari kwa mapambano.

Pia Gaddafi ametoa wito kwa nchi za Kiislamu kuunga mkono dhidi ya unyama huo unaofanywa na nchi za Magharibi.

Akizungumza kwa jazba, kiongozi huyo amesema wao, hawatajali kama mapambano hayo yatakuwa ya muda mfupi au mrefu, lakini hatimae wataibuka washindi.

Kauli hii imetolewa na Gaddafi katika Televisheni ya Taifa ya nchi hiyo baada ya zaidi ya wiki moja kuonekana hadharani.

"Tutapambana vilivyo katika vita hii vya kihistoria, hatutarudisha mioyo yetu nyuma, natoa miito kwa watu wote duniani nzima wasimame dhidi ya uvamizi huu"alisema Gaddafi.

Hata hivyo, serikali ya nchi hiyo imekanusha madai ya kuendesha operesheni ya mauji dhidi ya raia wa nchi hiyo kwa kusema kinachofanyika ni kujilinda dhidi ya waasi wanaotumia silaha.

Lakini waasi na baadhi ya wakazi wanasema, vikosi vinavyomuunga mkono Gaddafi vilivamia mji wa Misrata na kufanya mauwaji ya watu zaidi ya 40 juzi.

Aidha mashahidi wameendelea kusema kwamba jitihada hizo hazikuishia hapo,vikosi hivyo pia vilivamia mji mwingine wa Zintan uliyopo mpakani mwa nchi hiyo na Tunisia.

Ndege ya kivita ya majeshi ya Magharibi ikiwa katika operesheni
Ndege ya kivita ya majeshi ya Magharibi ikiwa katika operesheniPicha: AP

Hata hivyo, duru zinasema kwamba bado hakujawa na uhakika hasa wa taarifa hizo na nyingine nyingi kuhusu athari zinazotokea nchini Libya kwa sasa.

Wakati hali ni tete, Marekani tayari imetangaza kujiondoa katika uongozi wa operesheni hiyo.

Mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani, Ben Rhodes, amesema Marais Obama, Nicolas Sarkozy pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, wamekubaliana kwamba Umoja wa Kujihami wa NATO utaongoza mapambano hayo.

Rais Obama alisikika akisema "Mpaka atakapokuwa tayari kuondoka madarakani, bado kwa hivi sasa kitisho kwa raia wa Libya, tutaendelea na jitihada za kuwaunga mkono Walibya."

Wakati mijadala na matukio ya vita yakiendelea, raia nchini Libya wanajeruhiwa,wanapoteza maisha na wengine wengi wanaikimbia nchi hiyo.

Mhandishi: Sudi Mnette//DPAE/RTRE

Mhariri: Miraji Othman