1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gambari azungumza hatimae na Than Shwe

Oummilkheir2 Oktoba 2007

Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa arejea New York baada ya siku nne nchini Myanmar

https://p.dw.com/p/CH7K
Gambari na Aung San Suu Kyi
Gambari na Aung San Suu KyiPicha: AP

Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa Ibrahim Gambari amefanikiwa kuzungumza na kiongozi wa utawala wa kijeshi wa Myanmar Than Shwe katika mji mkuu mpya wan chi hiyo-Nyapyidaw.

Ibrahim Gambari,mwanadiplomasia wa kimataifa anaetokea Nigeria,ametwikwa jukumu na Umoja wa mataifa la kwenda Myanmar,baada ya maandamano ya amani ya watawa na umma kukandamizwa na watawala wa kijeshi mjini Rangoun.

Baada ya ingia toka na uvumi kuhusu afya ya kiongozi wa kijeshi wa Myanmar,hatimae mjumbe huyo maalum wa Umoja wa mataifa Ibrahim Gambari ameonana na Than Shwe katika mji mkuu mpya wa Myanmar-NYAPYIDAW.

Kiini cha mazungumzo yao lakini hakijulikani.

Wadadisi wanaamini Gambari amemuomba kiongozi huyo wa kijeshi mwenye umri wa miaka 74 asitishe visa vya ukandamizaji vinavyofanywa na vikosi vya usalama dhidi ya wananchi na akubali kuzungumza na kiongozi wa upande wa upinzani Aung San Suu Kyi.

Mjumbe huyo maalum wa Umoja wa mataifa ameshaondoka Myanmar ,baada ya kuzungumza kwa mara ya pili na mshindi huyo wa zawadi ya amani ya Nobel kwa mwaka 1991.

Ibrahim Gambari ameakhirisha mazungumzo aliyopangiwa kua nayo pamoja na wanadiplomasia walioko mjini Rangun,baada ya ziara hiyo ya siku nne.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Myanmar U Nyan Win akihutubia mbele ya baraza kuu la umoja wa mataifa amewatwika waandamanaji jukumu la kuvurugika hali ya mambo na kusema: “Vikosi vya usalama vilijizuwia kwa takriban mwezi mzima.Lakini maandamano yalizidi kupamba moto na yalikua ya uchokozi.Serikali ililazimika kupitisha amri ya watu kutotoka ovyo.Na amri hiyo ilipopuuzwa na waandamanaji,vikosi vya usalama vililazimika kuingilia kati kurejesha nidhamu.Hali imerejea kua ya kawaida hivi sasa nchini Myanmar.”

Idadi ya waliouliwa kufuatia maandamano hayo inahofiwa kupindukia watu 10 waliotangazwa na serikali ya kijeshi.

Wapinzani wa Myanmar wanaoishi nchi za nje wanazungumzia juu ya watu 100 walioliwa.

Waandamanaji 1700 wakiwemo watawa 500 wa kibudha na wanafunzi,wamekamatwa na kushikiliwa katika kambi moja ya serikali mjini Rangun.Na habari za hivi punde zinasema sheria za kutotoka ovyo saa za usiku,zilizotangazwa wiki iliyopita zimepunguzwa makali hii leo.

Uamuzi huo unaashiria ,utawala wa kijeshi unaidhibiti hali ya mambo,baada ya kuzwavunja nguvu waandamanaji.