1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gambia kujitoa katika Korti ya ICC Magazetini

Oumilkheir Hamidou
28 Oktoba 2016

Gambia na uamuzi wa kujitoa katika korti ya ICC ,Rwanda kutajwa kuwa mfano wa kuigizwa linapohusika suala la haki za wanawake na jeshi la Ujerumani Bundeswehr kuwajibika zaidi nchini Mali ndio mada kuu Magazetini

https://p.dw.com/p/2RpAF
Den Haag Internationaler Strafgerichtshof Prozess Jean-Pierre Bemba
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kooren

Tuanzie lakini moja kwa moja na uamuzi wa nchi ndogo ya Afrika Magharibi-Gambia wa kujitoa katika korti ya kimataifa ya uhalifu ICC mjini The Hague. Gazeti mashuhuri la Frankfurter Allgemeine linaandika:"Baada ya Afrika Kusini na Burundi,Gambia nayo imetangaza pia kujitoa katika korti hiyo ya mjini The Hague. Waziri wa habari Sheriff Bojang amesoma taarifa ya serikali kupitia televisheni ya nchi hiyo. Katika taarifa hiyo imetajwa kwamba Korti kuu ya kimataifa ya Uhalifu inalilenga bara la Afrika na viongozi wake" jambo ambalo serikali ya Gambia inasema "ni tusi kwa bara zima la Afrika".

 

Kadhia nane kati ya tisa zinazoshughulikiwa hivi sasa na korti hiyo ya ICC zinazihusu nchi za Afrika."Tangu ilipoanzishwa,visa visivyopungua 30 vya uhalifu wa vita vimefanywa na mataifa ya magharibi,bila ya kuandamwa" limeandika gazeti la Frankfurter Allgemeine,likimnukuu waziri wa habari wa Gambia,aliyekuwa akizungumzia vita vya Afghanistan,Iraq,Libya na Syria. Hata rais wa Uganda Yoweri Museveni ameitaja korti hiyo kuwa "haina maana yoyote" limeendelea kuandika Frankfurter Allgemeine linalohisi kujitoa Gambia ni pigo kwa mwendesha mashtaka mkuu Fatou Bensouda anaetokea katika nchi hiyo ya Afrika magharibi.

Miito ya kuifanyia marekebisho Korti ya ICC

Gazeti la Süddeutsche la mjini Munich,nalo pia limechambua uamuzi wa Gambia. Baada ya kusifu mandhari inayowavutia watalii na pia wimbi la wakimbizi wanaozama wakiwa njiani kuelekea Italy,Süddeutsche linazungumzia jinsi haki za binaadam zinavyovunjwa katika nchi hiyo inayotajikana kuwa miongoni mwa nchi masikini kabisa za dunia. Baada ya kuzungumzia pia uamuzi wa Burundi na Afrika Kusini kujitoa katika korti hiyo ya kimataifa,Süddeutsche imekumbusha pia kwamba mataifa mengi ya Afrika yametangaza azma ya kuchunguza uwezekano wa kujitoa. Hata hivyo limeutaja pia wito wa waziri wa sheria wa Senegal,Sidiki Kaba aliyezisihi nchi za Afrika,zisiipe kisogo taasisi hiyo na badala yake zishirikiane katika kuimarisha shughuli zake. Wito kama huo umetolewa pia na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Botswana aliyesema haoni sababu kwanini nchi za Afrika zijitoe katika korti hiyo ya kimataifa.

Rwanda mbele Ujerumani katika suala la usawa wa jinsia

Rwanda imegonga kwa mara nyengine tena vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani wiki hii;safari hii lakini inasifiwa kutokana na ile hali kwamba wanawake wanajivunia haki zaidi hata kupita Ujerumani-linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine."Ulimwengu ni mkubwa na haudhibitiki;kimoja lakini ni dhahir;linapaohusika suala la usawa wa jinsia-mabishano hayamaliziki-na hayatomalizika kwa muda wote ule ambao tofauti za kijinsia  zitaendelea kuwepo. Ikizingatiwa ripoti ya kongamano la kiuchumi duniani,mada hiyo itaendelea kuhanikiza angalao hadi mwaka 2186.

Hadi wakati huo utakapowadia,linaendelea kuandika gazeti la Frankfurter Allgemeine, watu watazidi kuduwaa kwa kuangalia takwimu zinazotolewa. Gazeti hilo linazungumzia faharasa za nchi 144 ulikofanyika uchunguzi kuhusu usawa wa jinsia-na katika orodha hiyo Ujerumani inakamata nafasi ya 13 na miongoni mwa nchi za viwanda hiyo ni nafasi nzuri kabisa. Ufaransa nafasi ya 17 ,Uingereza nafasi ya 20 na Marekani,hata bila ya Trump nafasi ya 45. Ujerumani lakini iko nafasi nane nyuma ya Rwanda ambayo ripoti ya kongamano la kiuchumi duniani inasema imeshakiuka asili mia 80 ya mstari unaoelekea usawa wa jinsia.

Bundeswehr kuimarisha shughuli za kulinda amani Mali

Ripoti yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika Magazeti ya Ujerumani wiki hii  imechambuliwa na gazeti la Süddeutsche na inahusu uamuzi wa jeshi la shirikisho Bundeswehr kuimarisha shughuli zake katika nchi inayokumbwa na mizozo ya Afrika Magharibi-Mali. Süddeutsche linanukuu duru za serikali zikithibitisha ripoti kwamba waziri wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinemeir na waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen wamekubaliana kimsingi kutumwa helikopta tangu za huduma za afya mpaka za kijeshi kuunga mkono shughuli za kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo inayokumbwa na machafuko. Süddeutsche linasema helikopta hizo zitaanza shughuli zake msimu wa kiangazi mwakani.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/presse

Mhariri: Mohammed Khelef