1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gauck ataka Ulaya ibainishe msimamo wake dhidi ya Trump

4 Februari 2017

Rais Joachim Gauck wa Ujerumani ametowa wito kwa Ulaya kuwa na msimamo wa wazi dhidi ya Rais Donald Trump wa Marekani kwa marufuku yake dhidi ya raia kutoka nchi zenye idadi kubwa ya Waislamu kuingia Marekani.

https://p.dw.com/p/2Wz4A
Bundespräsident Joachim Gauck
Picha: picture-alliance/dpa/S. Stache

Rais Joachim Gauck wa Ujerumani anayeondoka madarakani amehojiwa na magazeti matano ya Ulaya ambapo katika mahojiano hayo ametowa wito kwa Ulaya kubainisha msimamo wake dhidi ya marufuku ya rais mpya wa Marekani Donald Trump kuwazuwiya raia kutoka nchi saba za Kiislamu kuingia Marekani .

Gauck amesema "tunapaswa kuwa wazi kabisa juu ya suala hili".Wakati watu wenye imani ya Kiislamu na nasaba fulani wanapodaiwa kwa jumla ni hatari "hilo haliendani na dhana zetu za  utu wa binaadamu,usawa na uhuru wa dini."

Ikikabiliwa na ongezeko la sera kali za mrengo wa kulia barani Ulaya ametowa wito kwa wananchi kutoachiliwa peke yao na hofu zao wakati huu wa utandawazi na uhamiaji.

Sera kali za mrengo kulia kichocheo cha hofu

Deutschland Kabinettsumbildung Gauck mit Merkel und Steinmeier
Rais Joachim Gauck (katikati) Kanseka Angela Merkel na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje Frank-Waltrer Steinmeir.Picha: picture-alliance/AP Photo/M. SOhn

"Sera kali za mrengo wa kulia ni kichocheo cha hofu"amesema Gauck katika mahojinao hayo na kuongeza "majadiliano ya busara sio tu yataweza kuzuwiya hofu hizo bali hata tunahitaji majadiliano mazito zaidi, kukabiliana na zaidi na hofu hizo.Kwa ajili hii siasa inahitaji lugha ambayo sio tu inaeleweka na vigogo "hatuwezi kuachilia maneno rahisi yatumiwe na watu wa sera kali za mrengo wa kulia na wachochea hofu"

Kufuatia kujitowa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya Gauck ameonya kutoshinikiza kusonga mbele na kujumuishwa kwa mataifa katika Umoja wa Ulaya amesema Umoja wa Ulaya unahitaji kupunguza kasi hiyo yaani iwe hatua kwa hatua.Rais huyo anayeondoka madarakani ametaka siasa ichukulie kanuni ya usaidizi kwa umakini zaidi ni "mantiki zaidi kuratibu mambo katika ngazi ya taifa kuliko ngazi ya Ulaya hilo pia linapaswa kutokea" amesema.

Gauck amefanya mahojiano hayo na gazeti  la "NRC Handelsblad" la Uholanzi,"The Guardian" la Uingereza,"La Stampa" la Italia na "El Pais" la Uhispania .

Hapo Februari 12 mtu wa kuchukuwa nafasi yake atachaguliwa na bunge la Sirikisho la Ujerumani.Aliyekuwa Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeir wa chama cha (SPD) ana nafasi nzuri ya kuchaguliwa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/DW/dpa

Mhariri : Lilian Mtono