1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

McCain apitishwa rasmi.

Mtullya, Abdu Said4 Septemba 2008

Wajumbe kwenye mkutano wao mkuu wa chama cha Republican, unaofanyika St Paul Minnessota wamemteuwa rasmi John McCain kukiwakilisha chama hicho katika kugombea urais wa Marekani mwezi Novemba.

https://p.dw.com/p/FBMc
John McCain mgombea wa urais wa chama cha RepublicanPicha: picture-alliance / dpa

Hapo awali Gavana wa Alaska Sarah Palin alikubali kuteuliwa kuwa mgombea mwenza katika wadhifa wa makamu wa rais.

Wajumbe kwenye mkutano mkuu wa chama cha Republican wamemteua rasmi seneta John McCain kwa kura za kutosha kukiwakilisha chama hicho katika uchaguzi wa rais nchini Marekani utakaofanyika tarehe 4 mwezi Novemba.

John McCain atapambana na senata Barack Obama mgombea wa chama cha Demokratik.

Katika hotuba ya kusisimua ya kukubali kuteuliwa kuwa mgombea mwenzi, wa McCain gavana wa jimbo la Alaska, Sarah Palin alitumia wasaa wa hotuba hiyo kutetea hadhi yake na kumpigia debe John McCain. Palin amesisitiza msimamo wake wa kutetea mageuzi. Katika hotuba yake Palin pia alimshambulia mgombea wa chama cha Demokratik Barack Obama. Amesema Obama ni mtu mwenye kipaji cha kuwashawishi watu kwa maneno, lakini McCain ni mtu mwenye kipaji cha kuwashawishi watu kwa matendo.

Ameuliza jee Obama ana mpango gani kwa Marekani na anakusudia kufanya nini?

Gavana huyo amesema Obama anakusudia kuwachukulia watu fedha zaidi na kupunguza nguvu za Marekani katika zama ambapo dunia ni ya hatari.

Gavana Palin wa Alaska ameeleza kuwa Marekani inahitaji nguvu zaidi. Amesema ushindi unakaribia nchini Irak. Palin amemlaumu Obama kwa kutaka kukutana bila ya masharti, na wawakilishi wa serikali za kigaidi zinazowania kuwa na silaha za nyuklia.

Huku akishangiliwa kwa vifijo mama huyo mwenye umri wa miaka 44 aliendelea kumshambulia Obama kwa kusema kuwa katika siasa kuna wajumbe wanaotumia neno mabadiliko ili kuimarisha nyadhifa zao ;lakini amesema wapo wanasiasa kama McCain wanaotumia nyadhifa zao kuleta mabadiliko.


Baadae leo seneta McCain anatarajiwa kukubali rasmi kuteuliwa kukiwakilisha chama cha Republican katika uchaguzi wa rais. Seneta huyo wa Arizona mwenye umri wa miaka 72 atapanda mimbari katika siku ya mwisho ya mkutano mkuu wa chama cha Republican mjini St. Paul Minnesota.