1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GAZA CITY : Mawaziri wa Fatah watishia kujitowa serikalini

13 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBsC

Mawaziri kutoka kundi la Fatah wametishia kujitowa katika serikali ya umoja wa kitaifa ya Palestina iwapo mapigano yaliodumu kwa siku kadhaa kati ya kundi hilo na Hamas hayatosita.

Kamati kuu ya kundi hilo la Fatah imesema katika taarifa kwamba halitashiriki kwenye shughuli za serikali na kundi hasimu la Hamas.Mapigano kati ya wanamgambo wa kundi la Hamas la Waziri Mkuu Ismael Haniyeh na la Fatah la Rais Mahamoud Abbas yamesababisha vifo vya watu 37 katika kipindi cha masaa 24.

Saeb Erakat mshauri wa karibu wa Rais Abbas amesema anaamini ni kwa faida ya Wapalestina wote katika kipindi hiki kigumu cha historia yao kusimama imara na kwa majivuno kuuzima moto huo na kushikirikiana kurudisha serikali moja,silaha kuwa chini ya udhibiti mmoja na utawala wa sheria ambapo bila ya kufanya hivyo wote watakuwa wameangamia.

Mamia ya wapiganaji wa Hamas wakifyetuwa maroketi na mizinga wameteka makao makuu ya vikosi vya usalama vya Hamas kaskazini mwa Gaza hapo jana.

Rais Abbas amewashutumu viongozi wa Hamas kwa kupanga mapinduzi na kuna hofu kwamba mapigano kati ya makundi hayo yanaweza kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Wapalestina.