1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GAZA: Israel yafanya mashambulio zaidi dhidi ya wanamgambo wa Hamas

23 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBzB

Israel imefanya mashambulio zaidi ya angani dhidi ya wanamgambo wa chama cha Hamas katika Ukanda wa Gaza mapema leo. Wapalestina wasiopungua saba wamejeruhiwa kwenye mashambulio hayo.

Jeshi la Israel limesema ndege zake, zikiwa katika wiki ya pili ya kampeni ya mashambulio ya mabomu katika Ukanda wa Gaza, ziliyalenga majengo mawili yanayotumiwa na wanamagambo kutengeneza na kuhifadhi silaha.

Wapalestina wamekanusha madai hayo wakisema nyumba hizo hazikuwa zikitumiwa kuhifadhia silaha.

Habari zaidi zinasema wanajeshi wa Israel walifanya msako wa nyumba kwa nyumba katika eneo la kusini mwa Ukanda wa Gaza lililo karibu na mpaka na Misri. Wapalestina saba wamezuiliwa na kuhojiwa kwa muda kabla kuachiliwa.

Wanajeshi wa Israel wameonya watarudi tena katika eneo hilo na kuyaharibu makazi yote ikiwa maroketi yatavurumishwa kutoka eneo hilo kuelekea Israel.