1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GAZA: Jeshi la Israel lawashambulia wanamgambo

7 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCBn

Mtu mmoja ameuwawa na wengine wawili kujeruhiwa wakati helikopta za Israel zilipowashambulia wanamgambo wa kiislmau katika eneo la Ukanda wa Gaza.

Msemaji wa jeshi la Israel amesema wanajeshi waliokuwa ndani ya helikopta hizo walifyatua risasi wakati walipowaona watu wakitembea katika kivuko cha mpakani cha Jabaliya.

Jumapili iliyopita waziri wa ulinzi wa Israel, Amir Peretz, aliliamuru jeshi lianze tena operesheni zake katika Ukanda wa Gaza, hatua iliyokuwa imesitishwa tangu mwezi Novemba mwaka jana.

Sambamba na taarifa hizo, mapigano yamezuka tena kati ya makundi ya kipalestina yanayohasimiana katika Ukanda wa Gaza. Wanamgambo wawili na kijana mmoja wamejeruhiwa katika mapigano ya hivi punde baina ya wafuasi wa chama cha Hamas na chama cha Fatah.

Mapigano hayo yanafuatia tangazo la waziri mkuu wa serikali ya mamlaka ya Palestina, Ismael Haniyeh, kuitisha mkutano wa baraza la mawaziri hii leo kujadili mpango mpya wa usalama unaolenga kukomesha mapigano katika kipindi cha siku 100.

Licha ya kuundwa kwa serikali mpya ya umoja wa kitaifa, hali ya wasiwasi imeendelea kuwa mbaya baina ya chama cha Hamas na chama cha Fatah.