1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaza-Mapigano yanapamba moto

Oumilkher Hamidou4 Januari 2009

Idadi ya wahanga wa mashambulio inazidi kuongezeka

https://p.dw.com/p/GRpU

Gaza:


Idadi ya wahanga inazidi kuongezeka katika wakati ambapo vikosi vya nchi kavu vya Israel vinazidi kusonga mbele katika eneo linalodhibitiwa na Hamas-Gaza.Mashahidi wanasema jeshi la nchi kavu na vifaru wakisaidiwa na jeshi la wanaanga wanaendesha opereshini zao katika vitongoji vya mji mkuu wa Gaza.Mapigano makali yameripotiwa pia nje ya miji ya kaskazini ya Beit Lahiya,Beit Hanun na Jabaliya.Maafisa wa hospitali za wapalastina wanasema watu wasiopungua 30 wameuwawa na wengine 130 kujeruhiwa tangu vikosi vya Israel vilipovuka mpaka na kuingia Gaza jana usiku.Israel inasema wanajeshi wake 30 wamejeruhiwa,wawili kati yao ,wamejeruhiwa vibaya sana.Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak amewaambia maripota mjini Tel Aviv ,lengo kubwa la opereshini hii ya kijeshi ni kukomesha mashambulio ya papo kwa papo ya makombora ya Hamas dhidi ya Israel.Opereshini ya nchi kavu ya Israel imeanza siku nane baada ya hujuma za angani na baharini ambazo kwa mujibu bwa duru za wapalastina zimegharimu maisha ya watu wasiopungua 460 na zaidi ya 2700 kujeruhiwa.Katika kipindi hicho hicho,makombora yanayovurumishwa na Hamas yamewauwa waisrael wanne.