1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GAZA: Watu watatu wauwawa huko Gaza

19 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CChx

Watu watatu wameuwawa kwenye machafuko yaliyozuka upya leo katika Ukanda wa Gaza. Mapigano hayo yamezika matumaini ya kupatikana amani kati ya makundi hasimu ya Fatah na Hamas kufuatia makubailiano ya kusitisha mapigano yaliyoafikiwa juzi Jumapili.

Mapigano yameendelea mchana kutwa kati ya wafuasi wa chama cha Hamas na vikosi vya usalama vya rais Mahmoud Abbas.

Maofisa wawili wa usalama wa kikosi cha Fatah wameuwawa wakati wa ufyatulianaji wa risasi na wapiganaji wa Hamas. Afisa mmoja wa polisi wa Hamas aliuwawa katika mapigano yaliyozuka katika hospitali ya Shifa mjini Gaza.

Mbunge wa Palestina, Mustafa Barghouti, anataka mapigano yasitishwe.

´Tunataka mapigano haya yakome mara moja kwa sababu yanaharibu siku za usoni za wapalestina na waathiriwa wa mapigano haya ni wapalestina wa kawaida sio viongozi wa Hamas wala Fatah.´

Mapigano kati ya wafuasi wa Hamas na Fatah yameendelea kuongezeka tangu rais wa Palestina Mahmoud Abbas alipotangaza uchaguzi wa mapema mwishoni mwa juma lililopita.