1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gbagbo awekwa kizuizini

Halima Nyanza13 Aprili 2011

Rais wa Cote d'Ivoire Alassane Ouattara ameagiza kuwekwa katika kizuizi cha nyumbani kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Laurent Gbagbo ambaye ameng'olewa madarakani.

https://p.dw.com/p/10sMu
Laurent GbagboPicha: dapd

Serikali mpya ya Cote d'Ivoire imesema Laurent Gbagbo ambaye alikamatwa siku ya Jumatatu kutokana na kukataa kwake kuachia madaraka atabakia kizuizini.

Taarifa ilyotolewa na Waziri wa sheria wa nchi hiyo Jeannot Ahoussou-Kouadio, imesema Bwana Gbagbo pamoja na baadhi ya watu wake, bado wako kizuizini wakisubiri kuanza kwa uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.

Hata hivyo serikali ya Cote d'Ivoire haijasema ni wapi bwana Gbagbo anakoshikiliwa na pia watu wake hao wanaosubiri mashtaka pamoja naye wako wapi.

Alikamatwa pamoja na mke wake na mtoto wao wa kiume pamoja na maafisa wengine waandamizi wa serikali hiyo iliyong'olewa madarakani.

Serikali ya Rais Ouattara imesema Gbagbo atashtakiwa kuhusiana na mapigano yaliyoikumba nchi hiyo kwa miezi kadhaa, baada ya kukataa kukubali kwamba alishindwa katika uchaguzi wa Rais uliofanyika nchini humo, Novemba mwaka uliopita.

Kazi kubwa inayomkabili Rais Ouattara kwa sasa ni kukomesha machafuko katika ngome za Bwana Gbagbo, hususan katika mji mkuu wa nchi hiyo Abidjan.

Kumeripoti wa mapigano katika mji mkuu wa Abidjan, huku kukiwa na hali ya wasiwasi baada ya tetesi kwamba aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo Desire Tagro ambaye alikamatwa pamoja na Gbagbo, amekufa jana katika mazingira ambayo bado hayajafahamika.

Wafuasi wa Gbagbo wamedai kuwa Tagro aliuawa kwa risasi wakati akiwa kizuizini kwenye hoteli, ambayo Gbagbo alipelekwa mara tu baada ya kukamatwa, lakini hata hivyo duru za kidiplomasia zinasema kuwa inawezekana kuwa alitaka kujiua mwenyewe.

Mapigano katika mji huo wa Abidjan yamesababisha kuzagaa kwa miili ya watu waliokufa, mitaani na baadhi ya maeneo ya mji huo kukabiliwa na vitendo vya uporaji.

Hata hivyo hali inaonekana kuanza kurejea kawaida katika maeneo mengi ya mji huo, kwa magari kurejea tena barabarani na baadhi ya maduka kufunguliwa.

Katika hatua nyingine Rais wa Marekani Barack Obama ameahidi kumpa ushirikiano Rais Ouattara katika juhudi zake za kuiunganisha Cote d'Ivoire, na kuinua tena uchumi wa nchi hiyo, kurejesha usalama na kufanyia marekebisho jeshi la ulinzi la nchi hiyo.

Rais Obama alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Ouattara na kumpongeza hatimaye kuweza kushika madaraka hayo.

Wakati huohuo, majeshi ya Ufaransa na yale ya Cote d'Ivoire yamekuwa yakishika doria katika mji mkuu wa Cote d'Ivoire.

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Gerard Longuet ameliambia bunge la nchi hiyo kwamba wanajeshi hao watapiga doria katika mji huo ili kuonesha kuanza kwa utawala wa sheria.

Aidha amesema viongozi wa kijeshi na maafisa wa polisi waliokuwa wakimtii kiongozi wa zamani, Laurent Gbagbio wameahidi sasa kumtii Rais Ouattara.

Kikosi cha jeshi la Ufaransa kipo nchini humo kusaidiana na kikosi cha kulinda amani cha umoja wa Mataifa, kwa jukumu la kulinda wageni na kwamba vikosi vyote hivyo vilisaidia wapiganaji wa Ouattara kumkamata Bwana Gbagbo.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri:  Abdul-Rahman