1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gbagbo kusalimu amri ?

Halima Nyanza5 Aprili 2011

Ripoti zinasema kwamba Rais wa Cote d'Ivoire Laurent Gbagbo amekuwa akijadiliana juu ya kusalimu amri na kuachia madaraka, baada ya majeshi ya kiongozi wa nchi hiyo anayetambuliwa Kimataifa, kushambulia makazi yake.

https://p.dw.com/p/10nej
Rais Laurent GbagboPicha: AP

Balozi wa Cote d'Ivoire nchini Ufaransa ambaye ni mshirika wa Alassane Ouattara, Ally Coulibaly amekiambia kituo cha Televisheni cha Ufaransa kwamba bwana Gbagbo kwa sasa yuko katika mazungumzo kuona jinsi atakavyoweza kujisalimisha.

Amefahamisha kuwa Bwana Gbagbo bado yuko katika mji mkuu wa Abidjan.

Upande wa Gbagbo wapinga kusalimu amri:

Hata hivyo mshauri wa Rais Gbagbo mjini Paris, Ufaransa Tousssaint Alain amekanusha kwamba kiongozi huyo anampango wa kujisalimisha.

Ameongezea kusema kuwa bwana Gbagbo bado yuko hai na kwamba wala hajakamatwa na yupo katika makaazi hayo ya rais mjini Abidjan hata baada ya makaazi hayo kushambuliwa usiku wa kuamkia leo na kukiri kwamba uwezo wa jeshi la Gbagbo kwa sasa ni dhaifu.

Akisisitizia hilo msemaji wa Laurent Gbagbo amesema leo kwamba, majeshi yao yanaendelea kudhibiti makaazi hayo ya rais, nyumbani binafsi kwa rais Gbagbo pamoja na kambi kubwa ya jeshi iliyoko mjini Abidjan.

Aidha amesema Rais Gbagbo ameshangazwa na mashambulio ya moja kwa moja yanayofanywa na majeshi ya Ufaransa, wakati wakiwa bado katika majadiliano.

Ameongezea kusema kuwa mashambulio yaliyofanywa na Umoja wa mataifa na majeshi ya Ufaransa katika kambi mbili za jeshi zimeua watu wengi kutokana na kwamba wanajeshi wanaishi na familia zao katika kambi hizo.

Katika hatua nyingine Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa mataifa ambacho kinasaidiwa na jeshi la Ufaransa, kimekuwa kikilenga kuvunja nguvu uwezo wa silaha nzito wa Gbagbo kwa kufanya mashambulio ya helikopta hapo jana, baada ya raia kuuawa kwa mabomu katika siku za hivi karibuni.

Elfenbeinküste Unruhen nach Wahl
Mashambulio makali mjini AbidjanPicha: AP

Wakati huohuo, msemaji wa Umoja wa Mataifa nchini Cote d'Ivoire Hamadoun Toure amesisitiza kuwa Umoja wa mataifa umekuwa ukijaribu kuwalinda raia na sio kuegemea upande wa jeshi la Ouattara.

Kwa upande mwingine, Shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia haki za binadamu lenye makaazi yake mjini Geneva Uswisi limesema leo kwamba watu kadhaa wameripotiwa kuuawa katika siku za hivi karibuni, kutokana na utumiaji wa silaha nzito katika mapambano makali mjini Abidjan.

Msemaji wa shirika hilo Rupert Colville ameelezea wasiwasi wao juu ya hali iliyo katika mji huo unaokaliwa na mamilioni ya watu.

Afrika kusini nayo pia imeelezea wasiwasi wake juu ya machafuko hayo, hususani hali ya kibinadamu na kudorora kwa usalama, ambapo Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje Maite Nkoana-Mashabane ameutaka Umoja wa Afrika, Jumuia ya Uchumi ya nchi za Afrika magharibi ECOWAS na Umoja wa Mataifa, kutafuta ufumbuzi wa amani kuumaliza mzozo huo wa kisiasa.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters, afp)

Mhariri: Abdul-Rahman