1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Genge la wafuasi wa Maduro lawashambulia wabunge Venezuela

Caro Robi
6 Julai 2017

Magenge yanayoiunga mkono serikali ya Rais wa Venezuela Nicolas Maduro yalivamia bunge jana na kuwashambulia wabunge, ambapo wabunge saba walijeruhiwa katika vurumai hizo

https://p.dw.com/p/2g19w
Venezuela Sturm des Parlaments durch Anhänger von Nicolas Maduro
Picha: Reuters/A. Martinez

Wafuasi wa Rais Maduro walivamia bunge, kuwazuia kuondoka kwa masaa tisa wabunge 350, wahudumu wa bunge, wanahabari na wageni waliokuwa wakihudhuria kikao maalumu cha bunge cha kuadhimisha siku ya uhuru huku Polisi wakionekana kutoingilia kati kutuliza vurugu hizo bungeni.

Baadaye wanajeshi na polisi walifanya mzingiro kulizuia kundi hilo kuwashambulia wabunge na kuruhusu wabunge hao kuweza kuondoka bungeni. Tukio hilo ndilo la hivi punde katika mzozo wa kisiasa ambao umeikumba Venezuela kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita ambapo watu 90 wameuawa katika maandaamano ya karibu kila siku ya kuupinga utawala wa Maduro.

Wabunge kadhaa wajeruhiwa

Washambuliaji hao wasiopungua 100 waliokuwa wamejihami kwa fimbo, marungu, vipande vya  mabomba na hata mwingine kwa bunduki wanamuunga mkono Maduro ambaye anakabiliwa na shinikizo kutoka kwa upinzani aachie madaraka lakini Rais Maduro mwenyewe amelaani shambulizi hilo lililowalenga wabunge na kujitenga na vitendo hivyo.

Krise in Venezuela Überfall auf Parlament
Genge la wafuasi wa Maduro likiingia bungeniPicha: Picture Alliance/dpa/J. Cohen/Notimex

Awali Makamu wa rais Tareck El Aisaami aliwasili bungeni bila ya kutarajiwa akiwa ameandamana na mkuu wa majeshi Vladimir Padrino Lopez na mawaziri na katika hotuba yake aliwataka wafuasi wa Maduro  kuja bungeni kuonyesha kumuunga mkono Rais.

Spika wa bunge Julio Borges amemshutumu Rais Maduro kwa vurugu hizo na kuwashutumu maafisa wa usalama kwa kutochukua hatua kuzuia shambulizi hilo.

Shambulizi lalaaniwa vikali

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani pia imelaani uvamizi na vurumai hizo na kuzitaja shambulizi dhidi ya misingi ya kidemokrasia inayoenziwa na watu wa Venezuela waliopigania uhuru wa nchi hiyo miaka 206 iliyopita. Marekani pia imeshutumu kile ilichokitaja utawala wa unaozidi kuwa wa kimabavu wa Maduro. Colombia pia imelaani shambulizi hilo lililowalenga wabunge

Venezuela Nicolas Maduro
Rais wa Venezuela Nicolas MaduroPicha: Reuters/Handout: Miraflores Palace

Rais huyo wa Venezuela anashutumiwa kwa kusababisha mzozo wa kiuchumi ambao umepelekea mfumko mkubwa wa bei, uhaba mkubwa wa chakula, dawa na mahitaji mengine muhimu. Kwa upande wake Maduro  anaishutumu Marekani kwa kuunga mkono upinzani katika njama ya kutaka kumuondoa madarakani.

Huku hayo yakijiri, shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa takriban wanajeshi 123 wa Venezuela wamekamatwa tangu maandamano dhidi ya serikali yaanze mwezi Aprili kwa madai mbali yakiwemo uhaini, uasi, wizi na kuondoka jeshini.

Idadi hiyo ya wanajeshi waliokamatwa wa vyeo mbali mbali katika jeshi la majini, angani na la ardhini linatoa taswira ya kuwepo mgawanyiko katika Jeshi la Venezuela lenye wanajeshi 150,000.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters

Mhariri: Bruce Amani