1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

George Mitchell asisitiza juu ya uhalali wa kuweko dola ya Kipalastina

Miraji Othman12 Juni 2009

George Mitchell: Marekani haitazipa kisogo tamaa za Wapalastina kuwa na dola yao wenyewe

https://p.dw.com/p/I8IM
George Mitchell( kushoto), mwakilishi wa Marekani juu ya mzozo wa Mashariki ya Kati, akikutana na Rais wa Wapalastina, Mahmud Abbas, hivi karibuni mjini Ramallah, Ukingo wa Magharibi wa Mto JordanPicha: AP


Mwakilishi maalum wa Rais Barack Obama wa Marekani katika mzozo wa Mashariki ya Kati, George Mitchell, amesema Marekani inaunga mkono kuundwa dola ya Kipalastina kwa upesi kama iwezekanavyo. Pia ameihakikishia Lebanon kwamba juhudi za Marekani za kupata suluhisho la jumla kwa ajili ya mzozo wa Mashariki ya Kati, ikiwemo kuzifikia Syria na Iran, hazitafanywa kwa kuipa hasara Lebanon.

George Mitchell aliwaambia waandishi wa habari mjini Beirut hii leo kwamba Rais Barack Obama amebakia na ahadi yake ya kujishughulisha sana na kwa ukakamavu kutafuta amani jumla katika Mashariki ya Kati. Na jambo hilo ni pamoja na kuundwa dola ya Kipalastina, kama makaazi ya Wapalastina, tena kwa upesi kama iwezekanavyo. Aliyasema hayo baada ya kufanya mazungumzo na Rais Michel Suleiman na waziri mkuu, Fuad Saniora.

Alisema: Marekani haitoitoa mhanga Lebanon pale inapotafuta amani jumla katika Mashariki ya Kati. George Mitchell alisisistiza kwamba safari yake hii ya mwishoni katika eneo hilo, ambayo ilimchukuwa hadi Israel, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Misri na Jordan, pamoja na ziara za hapo kabla, ulikuwa ushahidi wazi kwamba utawala wa Rais wa Marekani, Barack Obama, umeahidi kujishughulisha vilivyo katika kutafuta amani ya eneo hilo. Hapo kabla alipokuweko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, George Mitchell alisema:

" Kama vile rais alivosema rais Obama wiki iliopita, Marekani haitazipa kisogo tamaa halali za Wapalastina za kuwa na heshima, nafasi na dola yao wenyewe."

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi wa Kipalastina, kuna wakimbizi wa Kipalastina baina ya 350,000 na 400,000 wanaoishi katika makambi 12 ya wakimbizi nchini Lebanon, nchi ilio na wakaazi zaidi ya watu milioni nne.

George Mitchell pia aliupongeza uchaguzi wa Juni 7 huko Lebanon na kuuita kuwa ni muhimu kwa ajili ya nchi hiyo, na akasema kwamba Marekani iko ngangari katika kuiunga mkono Lebanon ilio huru na yenye heshima ya mamlaka ya utawala wake.

Naye mwakilishi wa Wapalastina katika mashauriano ya amani ya Mashariki ya Kati, Saeb Erekat, anaamini kwamba Wapalastina sasa wako katika hali yenye nguvu kabisa, kisiasa, kuwahi kuonekana katika mzozo wao uliodumu miongo kadhaa na Wa-Israeli. Pia kunaonekana msimamo unaokubaliana ndani ya duru za Kipalastina na Kiarabu kwamba utawala wa Marekani mara hii unaweza kutoa zaidi kuliko kupiga porojo tu kuhusu tamaa za Wapalastina za kupata uhuru wao. Saeb Erekat alisema hivi:

" kusipotezwe tena zaidi wakati, sio kutumia mbinu za kuchelewesha mambo, masuala ni wazi kabisa kabisa, yako wazi. Nafikiri sasa ni wakati wa kuchukuwa maamuzi, sio wakati wa kushauriana..."

Hata jumuiya ya Hamas, ambayo ni hasimu mkubwa wa utawala wa ndani wa Wapalastina na inayoudhibiti Ukanda wa Gaza, imezungumzia kwa uzuri juu ya hatua za karibuni za Marekani, japokuwa jumuiya hiyo ina wasiwasi. Khaled Meshaal, mkuu wa Chama cha Hamas, anayeishi uhamishoni mjini Damascuss, alisema ametiwa moyo na lugha mpya ya busara ya Barack Obama, lakini alitahadharisha kwamba mtihani hauko katika lugha, lakini itategemea vipi maamuzi yanatekelezwa. Pia Meshaal alielezea wasiwasi juu ya namna Marekani ilivo sio wazi kabisa kuhusu ardhi ambayo itakuwa ya dola ya Kipalastina ya baadae, kurejea nyumbani wakimbizi wa Kipalastina, na Jerusalem ya Mashariki kuwa mji mkuu wa baadae wa dola ya Kipalastina.

Mwandishi: Miraji Othman AFP/IPS

Mhariri: Mohammed Abdulrahman