1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana baada ya uchaguzi wa duru ya pili ya urais.

Sekione Kitojo30 Desemba 2008

Maelfu ya wanaomuunga mkono mgombea wa upinzani John Atta Mills walijikusanya katika makao makuu ya tume ya uchaguzi mjini Accra, wakati tume hiyo ikijitayarisha kutangaza matokeo ya uchaguzi.

https://p.dw.com/p/GPRs
Wapiga kura nchini Ghana wakisubiri katika mstari kuweza kupiga kura zao kumchagua rais wa nchi hiyo katika uchaguzi wa duru ya pili, baada ya uchaguzi wa kwanza hapo Desemba 7 kushindwa kumpata mshindi.Picha: AP

Maelfu ya waungaji mkono mgombea wa chama cha upinzani John Atta Mills, wakiimba , mabadiliko , mabadiliko, waliizingira ofisi ya tume ya uchaguzi leo Jumanne wakati ikijitayarisha kutangaza matokeo ya uchaguzi wa rais wa duru ya pili ambapo matokeo yanakaribiana. Majeshi ya Usalama yamekuwa yakilinda ofisi hizo kabla ya kumtangaza mshindi.


Vyombo vya habari nchini Ghana vimetabiri ushindi mdogo kwa mgombea wa upinzani John Atta Mills, mgombea wa chama cha National Democratic Congress NDC dhidi ya mpinzani wake Nana Akufo-Addo wa chama tawala cha New Patriotic Party NPP kufuatia uchaguzi uliofanyika siku ya Jumapili katika taifa hilo la Afrika magharibi.

Wanajeshi wenye silaha pamoja na polisi , wakiwa na magari yenye mabomba ya maji, pamoja na magari ya deraya, yaliwaweka waungaji mkono wa chama cha upinzani cha NDC mbali na ofisi za tume ya uchaguzi mjini Accra.

Mkuu wa tume ya uchaguzi Kwandwo Afari-Gyan anatarajiwa kuwa na mkutano na waandishi wa habari baadaye leo kuhusiana na uchaguzi huo, ambao unafuatia uchaguzi wa duru ya kwanza hapo Desemba 7.

Matokeo ya awali yaliyotolewa hadi sasa na tume hiyo, ikiwa ni kura zilizohesabiwa kutoka majimbo 200 kati ya majimbo 250 nchini humo , yanaonyesha kuwa Atta Mills wa chama cha NDC akiwa anaongoza kwa asilimia 52.1 dhidi ya asilimia 47.9 za mgombea wa chama cha NPP Akufo-Addo.

John Atta Mills hata hivyo ameonya kuwa hatakubali matokeo yoyote mengine ya udanganyifu kutoka tume ya uchaguzi. Amesema kuwa ni muhimu kuheshimu matakwa ya wananchi na sio kujaribu kuweka kwa lazima mtu yeyote ili kuwatawala Waghana.

Polisi walifyatua risasi hewani jana jioni kuwatawanya waungaji mkono wa Mills wakati wakizingira jengo la tume ya uchaguzi.

Chama tawala cha NPP cha Akufo-Addo ambacho pia ni chama cha rais anayeondoka madarakani John Kufuor, kimepuuzia utabiri uliotolewa na kituo kimoja cha radio nchini Ghana Joy FM, ambacho kimekusanya matokeo kutoka katika vituo vya kupigia kura, na kutangaza kuwa Mills huenda akashinda.

Kumekuwa na baadhi ya ripoti za ghasia na hali ya kutokuwa na utulivu katika uchaguzi wa siku ya Jumapili. Lakini wengi wanamatumaini kuwa uchaguzi nchini Ghana unaweza kusaidia kurejesha heba ya demokrasia katika bara la Afrika, iliyochafuliwa na uchaguzi nchini Kenya na Zimbabwe pamoja na mapinduzi ya kijeshi nchini Mauritania na hivi karibuni Guinea.

►◄