1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana inamkumbuka Kwame Nkurumah

Zainab Aziz
5 Machi 2017

Wakati Ghana inajitayarisha kuadhimisha mwaka wa 60 tangu ijipatie uhuru wake mwanzilishi wa taifa Kwame Nkurumah anakumbukwa tena. Je ni kipi kilichobakia katika urithi aliouacha?

https://p.dw.com/p/2Yewe
Ghana Gründungsvater Kwame Nkrumah
Washiriki wa ngoma mbalimbali za asili kutoka katika maeneo tofauti nchini GhanaPicha: picture-alliance/dpa/T. Ridley

Jina la  Kwame Nkurumah wiki hii linaamsha mawazo na kuibua hisia mbalimbali miongoni mwa watu milioni 27 wa taifa la Ghana.  Atsu Aryee kutoka chuo kikuu cha Ghana ameiambia DW kwamba  jina la Nkurumah limefunikwa na usiri na utatanishi.  Lakini hali ilikuwa tofauti kabisa katika siku za mwanzo za utawala wake. Nkurumah alishangiliwa na umma wa Ghana kwa nderemo na vifijo pale nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Waingereza mnamo mwaka 1957.

Miaka michache baada ya uhuru wa Ghana

Ghana Kwame Nkrumah
Kwame Nkurumah mpiga vita ukoloni barani AfrikaPicha: imago stock&people

Miaka michache baada ya uhuru serikali yake ilianzisha mpango kabambe wa uchumi wa taifa hilo kwa lengo la kuigeuza nchi hiyo kuwa ya viwanda kwa kutegemea sana sekta ya kilimo.  Mradi wa mto Volta wa kuzalisha umeme bado ni chanzo kikuu cha umeme nchini Ghana lakini miradi mingine yote ilishindikana na mashirika ya umma aliyoyaanzisha yalisababisha madeni makubwa kutokana na ufisadi na uongozi mbovu.

Umma wa Ghana pia ulianza kushuhudia sura nyingine ya kiongozi huyo aliyekuwa mtetezi mkubwa wa uhuru.  Pole pole utawala wa Nkurumah ulianza kuwa wa kidikteta. Mnamo mwaka 1964 aliigeuza Ghana kuwa nchi inayotawaliwa na chama kimoja tu hatua iliyofuwatiwa na kujitangaza kuwa ni rais wa maisha.  Na hapo Waghana elfu 10 wengi wao wakiwa ni wasomi na watu mashuhuri walikimbilia nchi za nje. Hasira ziliendelea kujengeka miongoni mwa wananchi kutokana na uchumi kuzorota. Mnamo mwaka 1966 serikali ya Kwame Nkurumah ilipinduliwa na wanajeshi alipokuwa ziarani nchini China.

Umuhimu wa siasa za Nkurumah

Hata hivyo wataalamu wanasema siasa za Kwame Nkurumah zimesaidia kulijenga taifa la Ghana katika misingi ya utulivu uliopo hadi sasa. nchi hiyo haijawahi kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ikilinganishwa na nchi zilizo jirani ya Ghana licha ya kutokea mapinduzi ya kijeshi mara kadhaa katika miaka ya 70 na 80.  Atsu Aryee wa chuo kikuu cha nchini Ghana amesema urithi aliouacha Nkurumah ni utaifa na uzalendo aliouleta wakati alipokuwa madarakani. "Yaani kujitambua kuwa sisi ni Waghana na kwamba tuna nchi moja yenye utulivu". Lakini urithi huo unafifia.  Watoto wa shule wengi hadi hii leo bado wanajipanga foleni katika sehemu ambapo mwili wa kiongozi huyo umewekwa lakini ni wachache tu wanaofahamu Nkurumah alikuwa nani.

Muwakilishi wa wakfu wa Konrad Adenauer  wa nchini Ghana Burkhardt Hellemann amesema  jina la Kwame Nkurumah bado ni maarufu kwa sababu yeye ndiye aliyeongoza harakati za kupatikana kwa uhuru wa Ghana ijapokuwa vijana wengi hawajui yaliyotokea wakati wa utawala wa Nkurumah alipokuwa rais na waziri mkuu pia. Hellemann ameiambia DW kwamba mtu anaweza kuhisi jinsi jina la Kwame Nkurumah lilivyo bado na ushawishi ingawa ameeleza kuwa haoni dhana za kisiasa za Nkurumah kuwa na uzito katika mijadala ya siasa za kileo nchini Ghana.

Nkurumah alikuwa na imani kubwa juu ya dhana ya Uafrika. Alikuwa ni miongoni mwa viongozi waliokuwa na ushawishi barani Afrika.  Alitetea hoja ya kuleta Umoja wa Afrika ili kuzikabili siasa za nchi za magharibi.  Nkurumah alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Umoja wa nchi za Afrika.

Mwandishi: Zainab Aziz /http://dw.com/p/2YUK2

Mhariri: Sudi Mnette